Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imekubali kutoa hati ya wito wa kumleta Mahakamani Nargis Omar (70) ili aje asomewe mashtaka yanayomkabili.
Nargis anadaiwa kughushi wosia wa marehemu mama yake mzazi na kisha kujipatia nyumba kinyume cha sheria. Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu, Januari 6, 2025, na Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha ombi la kutaka mahakama hiyo itoe hati ya wito ili Nargis aletwe mahakamani.
Nargis anatakiwa kupelekwa mahakamani ili asomewe mashtaka yake, kisha aunganishwe na kaka yake, Mohamed Omar (64), ambaye alishafikishwa mahakamani Novemba 4, 2024, na kusomewa mashtaka mawili ya kughushi wosia wa mama yao.
Ombi hilo liliwasilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Neema Moshi, wakati kesi hiyo ya jinai ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake ukiendelea. Moshi alidai kuwa mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Nargis, aliruka dhamana ya polisi, hivyo wanaiomba mahakama itoe hati ya kumleta mahakamani ili asomewe mashtaka yake.
“Mheshimiwa Hakimu, tunaomba hati ya wito kwa mshtakiwa wa pili katika kesi hii, aletwe mahakamani hapa kumsomea mashtaka yake na kisha kumuunganisha na mwenzake,” alidai Wakili Moshi.
Hakimu Nyaki baada ya kusikiliza hayo, alikubaliana na upande wa mashtaka na kutoa hati ya wito wa kumleta Nargis mahakamani ili asomewe mashtaka yake. Baada ya kueleza hivyo, ameahirisha kesi hadi Februari 6, 2025, kwa kutajwa, na mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Mohamed, yupo nje kwa dhamana.
Katika kesi ya msingi, Mohamed alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Novemba 4, 2024, na kusomewa mashtaka mawili ya kughushi, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga.
Hata hivyo, siku hiyo mshtakiwa wa pili hakuletewa mahakamani kwa kile kilichoelezwa kuwa aliruka dhamana ya polisi. Kutokana na hali hiyo, upande wa mashtaka ulidai kuwa utamsomea mashtaka siku atakapokamatwa na kufikishwa mahakamani.
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kughushi wosia, tukio wanalodai kulitenda kati ya Julai 29, 1997, na Oktoba 28, 1998, Jijini Dar es Salaam. Inadaiwa kuwa washtakiwa walighushi wosia uliandikwa na marehemu Rukia Ahmed Omar, maarufu Rukia Sheikh Ali, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Shtaka la pili ni kuwasilisha nyaraka ya uongo mahakamani, tukio linalodaiwa kutendeka katika tarehe hizo katika Jiji la Dar es Salaam.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, Mohamed na dada yake Nargis, ambaye hajafikishwa mahakamani, walithibitisha uongo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kuwasilisha wosia unaodai kuwa marehemu mama yao, Rukia Ahmed Omar, alitoa nyumba moja kwa Nargis iliyopo kiwanja namba 35, eneo la Kariakoo, na nyumba nyingine kwa Mohamed iliyopo kiwanja namba 60, kitalu M, eneo la Magomeni, wakati wakijua kuwa ni uongo.