Bukoba. Maofisa 10 waandamizi wa kijeshi, kiraia na vyombo vya ulinzi na usalama kutoka ndani ya nchi na nchi rafiki, ambao ni wanachuo wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (NDC), wamepiga kambi ya mafunzo kwa vitendo mkoani Kagera kwa siku 10.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu, Januari 6, 2025, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (NDC), Meja Jenerali Wilberth Ibuge, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utaratibu wa chuo kwa maofisa waandamizi wanaoshiriki kozi za muda mrefu.
“Baada ya kipindi fulani cha masomo darasani, ni lazima wachukue sampuli ya baadhi ya mikoa na kuitembelea ili kujifunza kwa vitendo,” amesema Ibuge.
Amefafanua kuwa, kwa upande wa Kagera, chuo kimeleta washiriki 10 kati ya wanachuo 61 wa kozi hiyo na wengine wametawanywa kwenye mikoa mingine ya Ruvuma, Mtwara, Morogoro, Pwani, Njombe na Katavi.
“Ziara hii inalenga kuwafanya washiriki kuelewa utekelezaji wa sera na kuwawezesha kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu namna bora ya kuboresha na kutambua jitihada zinazofanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi,” amesema Meja Jenerali Ibuge.
Ameongeza kuwa chuo huchukua sampuli ya mikoa minane kati ya 26 ya Tanzania Bara ili kuangalia utekelezaji wa kisera, na baada ya Kagera, wataelekea mkoani Mara.
Kanali Bernad Mlunga, mmoja wa wanachuo hao ambaye kwa sasa anashiriki kozi ndefu ya kistratejia na kimkakati kundi la 18 kwa mwaka 2024/2025, amesema kozi hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na washiriki kutoka taasisi mbalimbali za Serikali.
“Baada ya kusoma darasani, nimefurahi kuona tunapata fursa ya kujifunza kwa vitendo mkoani Kagera. Tumeshuhudia shughuli nyingi za maendeleo, kama kilimo, uvuvi, ufugaji na utalii,” amesema Kanali Mlunga.
Amesema Mkoa wa Kagera una umuhimu wa kipekee kwa sababu unapakana na nchi za Uganda, Rwanda na Burundi, jambo linalowafanya washiriki kuangazia zaidi masuala ya uchumi wa mkoa na mchango wake kwa maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, amesema wamefurahi kuona mkoa wao umechaguliwa kuwa sehemu ya mafunzo hayo.
Amesema timu hiyo itapata fursa ya kutembelea maeneo ya kilimo, uvuvi na ufugaji, sambamba na kujifunza kuhusu masuala ya uchumi na ajira kwa vijana kulingana na jiografia ya mkoa huo.