Mawakala wa vyama vya siasa waonywa kuingilia uandikishaji wapigakura

Songwe. Mawakala wa vyama vya siasa wameonywa kuwaingilia maofisa uandikishaji wa daftari la kudumu la mpigakura litakaloanza hivi karibuni, bali wawe sehemu ya kutambua wapigakura kwenye vituo.

Wito huo umetolewa leo Jumatatu, Januari 6, 2025 na ofisa mwandikishaji Halmashauri ya Wilaya ya Ileje mkoani Songwe, Nuru Kindamba wakati akifungua mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura ngazi ya kata ambao wamekula kiapo cha kutunza siri wakati na baada ya kazi hiyo.

Kindamba amesema kazi hiyo inatakiwa ifanyike kwa weledi mkubwa, ikiwemo kwa kushirikiana na wadau wa uchaguzi ambao ni viongozi wa dini, mila na taasisi zisizo za kiserikali.

“Niwaombe sana mawakala wa vyama vya siasa, kazi hii itafanyika kwa siku saba kuanzia Januari 12 18, msije mkaingilia majukumu ya maofisa waandikishaji mkaleta vurugu, mkasimamie kazi ya kuwatambua raia wa Tanzania kwenye eneo lenu na kuacha kazi ifanyike kwa uhuru na  uwazi,” amesema Kindamba.

Pia ametumia nafasi hiyo kuwaomba wadau wa uchaguzi wilayani humo kuendelea kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpigakura, ili wawe na sifa za kushiriki uchaguzi mkuu mwaka huu.

Wakati hayo yakijiri wilayani Ileje, kwa Wilaya ya Mbozi, ofisa mwandikishaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Abdallah Nandonde amefungua mafunzo kwa watendaji wa uboreshaji daftari la kudumu la wapigakura ngazi ya kata na kuwasisitiza kufuatilia kwa umakini mafunzo hayo ambayo yamelenga kuwajengea uwezo wa namna ya kuendesha uboreshaji wa daftari hilo.

“Maofisa waandikishaji mnatakiwa kuifanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa kama zinavyoelekeza kanuni na sheria ili kufikia lengo lililokusudiwa kufanikisha kazi muhimu kwa Taifa na kujiepusha na vikwazo vinavyoweza kufifisha kazi hiyo,”amesema Nandonde.

Pia amewataka kuzingatia maelekezo ya tume yanayotolewa, huku akiwasisitiza juu ya kuwepo mawakala wa vyama vya siasa kwenye vituo, ingawa hawatakiwi kuingilia majukumu ya utekelezaji wake.

Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa a Uchaguzi (INEC), Dk Zakia Abubakari akizungumza wakati wa mafunzo hayo wilayani Ileje,  amesema ili kufanikisha kazi ya uandikishaji kwa weledi ni muhimu kuwepo ushikiano wakati wote baina ya maofisa waandikishaji ngazi ya kata na vijiji, halmashauri na tume pamoja na wadau wote wa uchaguzi, ili lengo la kuandikisha wapigakura wapya zaidi ya milioni tano litimie.

Related Posts