Okutu aweka ngumu Pamba Jiji

KITENDO cha mabosi wa Pamba Jiji kutaka kumtoa kwa mkopo mshambuliaji wa timu hiyo, Eric Okutu, kambi ya mchezaji huyo Mghana imeibuka na kudai haikubaliani na jambo hilo, isipokuwa kwa sharti moja la kuuvunja mkataba uliobaki wa miezi sita.

Viongozi wa Pamba wanahitaji kumpeleka Okutu kwa mkopo KenGold na hii ni baada ya kuinasa saini ya mshambuliaji Mkenya, Mathew Tegisi Momanyi kutoka Shabana, ingawa raia huyo wa Ghana inaelezwa hajakubaliana na suala hilo kwake.

Akizungumza na Mwanaspoti, Okutu alisema hana taarifa juu ya kutolewa kwa mkopo kwani anachokifahamu bado ana mkataba wa miezi sita na kikosi hicho, huku akiweka wazi hana dhamira yoyote ya kuondoka labda itokee ofa kwa timu nyingine za nje.

“Bado nina mkataba na Pamba na siwezi kuzungumzia zaidi ya hapo, suala la kutolewa kwa mkopo nimelisikia ingawa sijapewa barua rasmi juu ya hilo, ikitokea nitaweka wazi kwa sababu yapo makubaliano yetu tuliyokubaliana mwanzoni,” alisema.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Pamba, Ezekiel Ntibikeha alisema maboresho yoyote yatakayotokea ndani ya kikosi hicho watayaweka wazi, kama walivyoanza kutangaza usajili wa mastaa wapya waliowasajili katika dirisha hili.

Sababu za nyota huyo kutaka kutolewa ni kutokana na kukorofishana na kocha wa timu hiyo, Fred Felix ‘Minziro’, baada ya kujibizana naye kufuatia kuonyeshwa kadi nyekundu katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons Desemba 26, mwaka jana.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya na wenyeji kushinda bao 1-0, Okutu alionyeshwa kadi hiyo ikiwa ni muda mfupi tangu aingie akichukua nafasi ya Samuel Antwi, baada ya kumchezea madhambi beki wa Prisons, Michael Ismail Mpesa.

Kitendo kilichofanywa na nyota huyo kilionekana kumuudhi Minziro.

 Minziro aliwataka viongozi kumchukulia hatua za kinidhamu, kwa kile alichodai alishusha zaidi morali ya wachezaji wenzake ya kupambana na kusababisha kupoteza mchezo huo muhimu.

Nyota huyo amejiunga na timu hiyo msimu huu baada ya kuachana na Tabora United aliyojiunga nayo mara ya kwanza msimu wa 2023-2024 akitoka Hearts of Lions ya Ghana na akiwa na kikosi hicho cha Nyuki wa Tabora, alikifungia mabao saba ya Ligi.

Related Posts