Ongezeko la uwekezaji sekta ya utalii lakuza uchumi Z’bar

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, amesema kuna ongezeko kubwa la wawekezaji katika sekta ya utalii, hatua inayochangia kukuza uchumi na kuleta maendeleo nchini.

Amesema ongezeko hilo hasa katika uwekezaji wa hoteli, linachangia kuvutia idadi kubwa ya watalii wanaotembelea Zanzibar, hivyo kukuza sekta ya utalii.

Dk Mwinyi amesema hayo leo Jumatatu Januari 6, 2025, wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hoteli ya SSPD-Buhairan Bwejuu, iliyopo Mkoa wa Kusini Unguja, inayomilikiwa na wawekezaji kutoka Falme za Kiarabu.

“Uwekezaji huu unakuza utalii na faida zake ni kubwa katika nyanja mbalimbali za kiuchumi. Hivyo, nawahimiza wananchi tuendelee kuwaunga mkono wawekezaji wanaowekeza katika maeneo yetu,” amesema Rais Mwinyi.

Amesema pamoja na fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, uwekezaji huo utatoa soko la bidhaa za wakulima na wavuvi, hasa mazao ya baharini hali itakayochangia kuongezeka kwa pato la Taifa.

“Kila mtu anafahamu kuwa, sekta ya utalii kwa sasa inachangia takriban asilimia 30 ya pato la Taifa la Zanzibar, na ndiyo maana inachukuliwa kama sekta mama,” amesema Dk Mwinyi.

Akizungumzia viwango vya hoteli hiyo, Rais Mwinyi amesema kufunguliwa kwake kutafungua milango kwa Zanzibar kupokea wageni wengi zaidi kutoka Falme za Kiarabu.

Aidha, amewapongeza wananchi wa Bwejuu na Mkoa wa Kusini kwa kuonyesha utayari wa kuwakaribisha wawekezaji, akisisitiza umuhimu wa kushirikiana nao ili kuinua pato la Taifa na kuongeza ajira kwa vijana.

“Wananchi wetu wanapaswa kuwa na utayari na uvumilivu wa kushirikiana na wawekezaji ili kukuza vipato vyao na kutoa nafasi za ajira kwa vijana wetu,” amesisitiza Rais Mwinyi.

Wakati huohuo, Rais Mwinyi ameridhia ombi la Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Muhammed Mahmoud la kutengenezwa barabara ya kilomita tatu kwa kiwango cha lami kutoka Michamvi Mashariki hadi Michamvi Magharibi.

Kwa upande wake, Dk Muhammed Omar akizungumza kwa niaba ya mmiliki wa mradi wa ujenzi wa Hoteli ya SSPD-Buhairan Bwejuu, ameishukuru Serikali kwa kuruhusu uwekezaji huo.

Amesema mradi huo utatoa ajira zaidi ya 500 na kuchangia uchumi wa nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Saleh Saad Muhammed amesema kwa miaka minne ya Awamu ya Nane, mamlaka hiyo imesajili takribani  miradi 430 ya uwekezaji yenye thamani ya Dola 5.6 bilioni za Marekani, inayotarajiwa kutoa ajira 25,000.

Ufunguzi wa mradi huo ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Related Posts