Raia watatu wa Israel wauawa Ukingo wa Magharibi – DW – 06.01.2025

Watu wenye silaha walilifyatulia risasi hii leo basi lililokuwa limebeba Waisraeli katika kijiji cha cha Al-Funduq karibu na makazi ya walowezi ya Kedumim kwenye Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na kuua watu wasiopungua watatu na kuwajeruhi wengine saba.

Mkuu wa kitengo cha polisi cha Israel katika Ukingo wa Magharibi Moshe Pinchi amesema uchunguzi unaendelea.

” Ni shambulio baya, na cha kusikitisha ni kwamba raia wamelipa gharama kwa maisha yao. Kwa sasa, tuko katika hatua za kuchunguza tukio hili, tunalichunguza eneo liliko-tokea, pamoja kwa kushirikiana na jeshi la Israel, Polisi na Idara ya usalama wa taifa na hatimaye tutawatambua waliohusika.”

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Picha: Uncredited/Israeli Government Press Office/AP/dpa/picture alliance

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kuwa wahusika wa shambulio hilo na yeyote aliyewasaidia watawajibishwa na kwamba hakuna atakayeepuka. Hamas wamepongeza shambulio hilo katika taarifa yao lakini hawakudai kuhusika.

Soma pia: Israel inaendeleza vita vyake dhidi ya wanamgambo katika Ukingo wa Magharibi

Ghasia zimeongezeka eneo hilo tangu kuanza kwa vita vya Gaza ambapo Israel imekuwa ikiendesha operesheni za mara kwa mara kwa madai ya kuwasaka wale inaowaita “wapiganaji na magaidi” huku Wapalestina nao wakijibu kwa kushambulia kwa risasi na vilipuzi. Wizara ya Afya ya Palestina imesema takriban Wapalestina 838 wameuawa na Israel katika  Ukingo wa Magharibi  tangu wakati huo.

Na huko Gaza, mamlaka zinaeleza kuwa ndani ya muda wa saa 24 zilizopita, watu 49 wameuawa kufuatia mashambulizi ya Israel. Pia kunaarifiwa kuwa roketi tatu zilifyetuliwa kutoka Gaza kuelekea Israel, huku moja ikifanikiwa kuipiga nyumba moja katika mji wa mpakani wa Sderot.

Matukio hayo kukwamisha mpango wa amani?

Viongozi wa Marekani na wale wa mataifa ya kiarabu wakiujadili mzozo wa Gaza
Viongozi wa Marekani, Misri , Qatar na wengine wa mataifa ya kiarabu wakiujadili mzozo wa GazaPicha: JONATHAN ERNST/AFP

Hayo yanajiri huku kukiwa na msukumo wa kidiplomasia unaolenga kufikiwa makubaliano ya kusitisha vita vilivyodumu kwa miezi 15 huko Gaza na kuwaachilia mateka wa Israel.

Soma pia: Netanyahu ataacha urathi gani baada ya vita vya Gaza?

Matukio haya yanaweza kuwa kikwazo cha ziada cha kufikiwa kwa mpango huo licha ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kusema hivi leo kuwa ana matumaini kwamba mpango huo unakaribia kufikiwa.

Hata hivyo Israel imesema Hamas bado haijazungumzia chochote kuhusu mateka 34 ambao kundi hilo lilitangaza kuwa tayari kuwaachilia huru katika awamu ya kwanza ya makubaliano ya kubadilishana mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina.

(Vyanzo: AP, DPA, AFP)

Related Posts