WAKATI Singida Black Stars ikirejea mazoezini chini ya kocha mpya, Miloud Hamdi mwenye uraia wa Ufaransa na Algeria, mabosi wa timu hiyo wako katika hatua za mwisho za kumnasa beki wa kulia wa Gor Mahia ya Kenya, Rooney Onyango.
Nyota huyo aliyejiunga na GorMahia 2022 akitokea Wazito FC anatarajia kujiunga na Singida Black Stars katika dirisha hili dogo la usajili ikielezwa anaenda kuwa mbadala wa beki Israel Mwenda aliyetua Yanga.
Katibu Mkuu wa GorMahia, Sam Ocholla amethibitisha taarifa za beki huyo kuondoka kikosini akiweka wazi makubaliano baina ya klabu hizo mbili yamefikiwa rasmi, hivyo kilichobaki ni mchezaji mwenyewe kukubaliana maslahi binafsi.
“Mchezaji alitutaarifu amefikia makubalino binafsi na Singida wiki chache zilizopita na sisi pia tulifanya jitihada za kuongea nao na kuona hakuna tatizo, tumuache aende na ataondoka mwezi huu. Tunamtakia heri aendako,” alisema Ocholla.
Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza alipotafutwa kuzungumzia usajili wa nyota huyo, alisema kukiwa na taarifa rasmi kama klabu wataitoa, ingawa maboresho ya kikosi hicho bado yanaendelea.
Rooney aliyetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Kenya mara mbili akiwa na Gor Mahia akicheza timu mbalimbali zikiwemo za Thika United, Shabana FC, Gusii United na kikosi cha Kenya ‘Harambee Stars’, anatajwa miongoni mwa mabeki bora wa kulia.
Nyota huyo mwenye miaka 23, alitabiriwa makubwa hasa baada ya kucheza mchezo wake wa kwanza na kuonyesha uwezo mkubwa akiwa Harambee Stars iliyolazimishwa sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Russia Oktoba 16, 2023.
Hata hivyo, licha ya ubora wake lakini anatakiwa kufanya kazi ya ziada kupenya katika kikosi cha kwanza cha Singida Black Stars kutokana na uwepo wa beki raia wa Ivory Coast, Ande Koffi Cirille ambaye amekuwa mhimili mkubwa wa timu hiyo akiwa ndiye panga pangua katika kikosi.
Cirille aliyejiunga na Singida msimu huu akitokea Asec Mimosas ya kwao Ivory Coast, amekuwa miongoni mwa mabeki bora wa kikosi hicho hadi sasa wanaocheza upande wa kulia, huku akichangia mabao matatu ya Ligi Kuu kati ya 22 ya timu nzima.