Sababu ACT kuiburuza Tamisemi mahakamani

Dar es Salaam. Malalamiko dhidi ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Novemba 27, 2024 hatimaye yamefikia hatua ya mahakamani, baada ya Chama cha ACT Wazalendo kufungua mashauri 51 kupinga matokeo na mwenendo wake.

Hatua hiyo ya ACT Wazalendo inakoleza moto wa malalamiko dhidi ya uchaguzi huo, yaliyoibuliwa na vyama vya upinzani na baadhi ya wadau wa siasa, wakidai ulikuwa na kasoro mbalimbali zikiwemo za kuenguliwa kwa wagombea wa upinzani na kuingizwa kwa kura feki.

Kutokana na mienendo hiyo, ACT Wazalendo iliwahi kutoa wito wa uchaguzi huo urudiwe, huku Chadema kikikataa kuyatambua matokeo na kuweka msimamo wa kutofanyika chaguzi zozote bila mabadiliko ya sheria ikiwemo Katiba.

Kasoro za uchaguzi huo, hazikuishia kutajwa na vyama vya siasa pekee, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba naye aliviambia vyombo vya habari, yaliyofanyika katika uchaguzi huo yamefuta matumaini ya wananchi juu ya kuimarika kwa demokrasia.

“Yale yaliyotokea 2019 na 2020, mchakato uliopo ambao tumeumaliza sasa hivi yametokea yale yale. Yametokea yale yale na chanzo chake zaidi ni wasimamizi wenyewe wa uchaguzi.

“Hili kwangu ndiyo naliona kama tukiendelea na utaratibu huu tunajenga mazingira ya kuja kuleta vurugu ambayo itakuja kuhatarisha amani yetu,” amesema.

Katika uchaguzi huo, CCM ilipata ushindi wa asilimia 99.01, Chadema asilimia 0.79, ACT Wazalendo asilimia 0.09, CUF asilimia 0.08 na NCCR Mageuzi asilimia 0.01.

Hata hivyo, baada ya hatua hiyo ya ACT Wazalendo Mwananchi ilimtafuta Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa na Katibu Mkuu wake, Adolf Ndunguru lakini simu zao ziliita bila kupokelewa.

Kwa upande wake, Mwanasheria Mwandamizi wa Tamisemi, Mihayo Kadete amejitenga na sakata hilo huku akisema wanaoshtakiwa si Tamisemi bali ni halmashauri husika  kwa kuwa walikuwa wasimamizi wa sehemu husika.

“Halmashauri zilizotajwa wao ndiyo wana hizo taarifa za hizo kesi, Tamisemi tulikuwa waratibu tu lakini waliokuwa wanasimamia uchaguzi walikuwa halmashauri. Kesi hawajaishtaki Tamisemi wamezitaja waliowashtaki huko halmashauri,” amesema Kadete.

Katika taarifa ya ACT Wazalendo iliyotiwa saini na Mwanasheria Mkuu wake, Omar Said Shaaban chama hicho kimesema kimeshafungua mashauri 51 kupinga matokeo na mwenendo wa uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024.

“Kesi hizo zimefunguliwa katika mahakama za wilaya mbalimbali za Tanzania Bara na tayari zimeshaanza hatua za awali ambazo ni kutolewa wito wa mahakama kuwaita wahusika kwa ajili ya kutajwa na kujibu mashauri,” imeeleza taarifa hiyo.

Ilizitaja Wilaya ambazo mashauri hayo yamefunguliwa ni Temeke, Lindi, Ilala, Momba, Mkuranga, Mafia, Kigoma, Tunduru, Tandahimba, Kilwa na Kibiti.

Chama hicho kimeeleza kuwa kimeshapanga mawakili wa  kusimamia kesi zote.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua ya kufungua mashauri hayo ni mwendelezo wa dhamira ya kupigania demokrasia na haki za wananchi zilizoporwa wakati wa uchaguzi huo.

“Katika hatua ya sasa tunatoa wito kwa wanachama na wapenzi wote wa demokrasia nchini kujitokeza kwa wingi wakati wa kesi hizi zinapoitwa mahakamani na chama kitaendelea kutoa taarifa ya kila hatua katika mwenendo wa mashauri haya,” imeeleza taarifa hiyo.

Akizungumzia uamuzi huo, Mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Iddi Mandi amesema ni sawa kwa chama hicho kwenda mahakamani iwapo hakikuridhishwa na mchakato na matokeo ya uchaguzi husika.

Hata hivyo, amesema kingine kinachoipa ACT Wazalendo uhalali wa kwenda mahakamani ni Katiba ya nchi, iliyoweka wazi kuwa, uchaguzi pekee usiopaswa kupingwa mahakamani ni wa Rais.

“Katiba inakataza uchaguzi wa Rais pekee ndiyo usipingwe mahakamani, lakini uchaguzi wa wabunge, madiwani na serikali za mitaa unaweza kupingwa mahakamani,” amesema.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk Revocatus Kabobe amesema hukumu ya mahakama ndiyo itakayoamua ukweli unaobishaniwa baina ya  upinzani na CCM.

Amesema CCM imekuwa ikijisifu kwa kusema imeshinda uchaguzi ulioendeshwa kwa mazingira huru na haki, huku upinzani ukisema kulikuwa na kasoro lukuki, kitakachoamriwa na mahakama kitahalalisha hoja za moja kati ya pande mbili.

“Ikitokea mahakama ikasema uchaguzi ulikuwa wa haki, basi itakuwa nzuri kwa CCM, lakini mahakama ikija na hukumu itakayosema kulikuwa na kasoro, basi madai ya upinzani yatakuwa na mashiko na ushindi wa CCM, utakuwa na mashaka,” amesema.

Hata hivyo, amesema ipo historia ya kuwahi kufunguliwa mashauri mahakamani ya kupinga chaguzi na zikafanyika upya, hivyo kuna uwezekano wa hilo kutokea kwa uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Mahakama ndicho chombo cha mwisho ha kutoa haki, malalamiko yao ACT Wazalendo yatajibiwa mahakamani,” amesema.

Related Posts