Njombe. Jana tulikuletea tuhuma za mauaji zilivyokuwa dhidi ya kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), George Sanga na wenzake wawili, walioshikiliwa mahabusu.
Hii ni baada ya kukaa mahabusu siku 1,557 tangu walipokamatwa Septemba 26, 2020 kwa tuhuma za mauaji ya kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Emmanuel Mlelwa hadi walipoachiwa huru na Mahakama Desemba 31, 2024.
Mbali na Sanga, makada wengine walioachiwa huru ni Goodluck Oygen maarufu Mfuse aliyekuwa mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo na Optatus Nkwera aliyekuwa mshitakiwa wa tatu.
Leo tunaendelea kukuletea simulizi za hukumu ya kesi hiyo iliyotolewa na Jaji Dunstan Ndunguru wa Mahakama Kuu Kanda ya Njombe aliyewaona washtakiwa hawana hatia na kuamuru waachiwe huru.
Shahidi wa sita wa Jamhuri, Koplo Angelo mwenye namba G.8387 aliieleza Mahakama kuwa Septemba 21, 2020 yeye, mkuu wa upelelezi wilaya (OCD) na polisi wengine walivyoshuhudia mwili wa marehemu.
Upekuzi nyumbani kwa Sanga
Alieleza kuwa, Septemba 27, 2020 alipangiwa kazi ya kufanya upekuzi nyumbani kwa mshitakiwa wa kwanza, Sanga na alipata fulana mbili za Chadema na ilikuwa na matone ya damu.
Shahidi huyo alieleza kuwa, alipata taarifa kuwa gari aina ya Toyota Gaia yenye namba T456 DAB aliipekua na kupata mkanda wenye rangi ya damu ya mzee ukiwa katika viatu mithili ya jeshi au boot.
Siku hiyo pia, alipewa jukumu la kuandika maelezo ya onyo ya mshitakiwa wa tatu, Nkwera na katika maelezo hayo alidai, mshitakiwa alikiri kushiriki kumuua marehemu na kuwataja wengine ni Sanga, Mfuse na Ashery.
Mbali na kazi hiyo, Septemba 29, 2020 walienda eneo la tukio kwa kuongozwa na mshitakiwa wa kwanza na alichora ramani ya eneo hilo, lakini Konstebo Hekima alichukua sampuli za DNA kutoka kwa mshitakiwa huyo.
Shahidi wa saba, Sajenti Bedon mwenye namba F.3845 alieleza namna yeye na maofisa wenzake walivyomkamata mshitakiwa wa tatu huku shahidi wa nane, Geofrey Mgaya akielezea alivyoshuhudia upekuzi nyumbani kwa Sanga.
Kwa upande wake, shahidi wa tisa, Inspekta John Mapuga alieleza namna Septemba 27,2020 alivyopewa amri ya kumkamata mshitakiwa wa pili, Mfuse na kumpeleka kituoni na siku ya pili alifanya upekuzi nyumbani kwake.
Shahidi huyo alidai kuwa, katika upekuzi huo alipata kitambaa cha kujifutia kilichokuwa na matone ya damu na suruali mbili; moja ya rangi ya blue na nyingine nyeusi, fulana rangi ya kijivu na sweta moja.
Vitu vyote hivyo vilitolewa na kupokewa mahakamani kama vielelezo.
Shahidi wa 10, Koplo Hekima mwenye namba G.5938 ambaye ni polisi mchunguzi wa kisayansi, alidai kwamba Septemba 21,2020 aliagizwa kwenda Hospitali ya Kibena kuchukua sampuli za DNA.
Sampuli hizo zilitoka katika mwili wa marehemu uliokuwa chumba cha kuhifadhia maiti na alichukua sampuli ya damu kutoka puani na kwenye sikio kisha alizikausha na kwenda kuzihifadhi kwenye kabati maalum.
Septemba 29, 2020 alichukua sampuli kutoka kwenye fulana sare ya Chadema ya mshitakiwa Sanga iliyokuwa na matone ya damu na pia akachukua sampuli kutoka kitambaa cha mshitakiwa wa pili kilichokuwa na matone ya damu.
Pia, alichukua sampuli za DNA (mpanguso) kutoka mdomo wa mshitakiwa wa kwanza na akafanya hivyo kutoka kwa Thadey Mwanyika na hivyo hivyo kwa mshitakiwa wa pili (Mfuse) na kumkabidhi Koplo Angelo.
Shahidi wa 11, mkaguzi msaidizi wa Polisi, Isaya Benard alielezea namna alivyotolewa makao makuu ya Polisi Dar es Salaam na kwenda Njombe kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa sampuli za DNA.
Kwa upande wake, shahidi wa 11, Koplo Judica mwenye namba H.8133 alielezea namna alivyopokea vielelezo mbalimbali na kuvihifadhi ambavyo ni fulana, sare ya Chadema na kitambaa vikiwa na matone ya damu.
Shahidi wa 13 alikuwa John Joshua aliyekuwa mwenyekiti wa mtaa ambaye alisema aliitwa na polisi kama shahidi huru kushuhudia upekuzi nyumbani kwa mshitakiwa wa pili (Mfuse) na kitambaa chenye damu kilipatikana.
Ukiacha ushahidi huo, shahidi wa 14, Koplo Peter mwenye namba H.1913 alidai kuwa Septemba 26, 2020 saa 12:00 jioni aliandika maelezo ya onyo ya mshitakiwa wa kwanza na kudai alikiri kushiriki kumuua Mlelwa.
Alielezea kile alichodai kuwa, mshitakiwa alimwelezea namna alivyopata taarifa kutoka kwa Mwanyika kuhusiana na marehemu kufanya mchezo mchafu wa kuwashawishi wagombea wa Chadema wajiengue ili CCM wapite bila kupingwa.
Shahidi huyo alidai, mshitakiwa alimweleza namna walivyopanga kumuua marehemu na namna walivyotekeleza mpango huo, lakini alipojaribu kuyatoa maelezo hayo mahakamani kama kielelezo, yalikataliwa.
Sanga alivyojitetea kortini
Baada ya kusikiliza ushahidi wa Jamhuri, Mahakama iliwaona washitakiwa wana kesi ya kujibu, hivyo kutakiwa kujitetea na walijitetea chini ya kiapo.
Mshitakiwa wa kwanza, Sanga alieleza kuwa alikamatwa Septemba 26,2020 akiwa kituo cha polisi na Emmanuel Masonga na Rose Mayemba walipokwenda kuulizia ni kwanini Thadey Mwanyika anashikilia na polisi.
Baada ya kukamatwa, alipelekwa kituo cha Polisi Makambako ambako alipigwa na polisi, lakini akiwa hapo hakuwahi kuhojiwa na alikuja kufahamu anakabiliwa na tuhuma za mauaji aliporudishwa kituo cha Polisi Njombe na kupelekwa kortini.
Alipofikishwa kortini ndipo alipokutana na washitakiwa wenzake na kueleza kuwa hakuwahi kukiri kutenda kosa hilo mbele ya Koplo Mrisho aliyekuwa shahidi wa nne wa Jamhuri na Koplo Peter aliyekuwa shahidi wa 14 wa Jamhuri.
Alieleza kuwa siku ya tukio la mauaji, yeye alikuwa kata ya Ihanga na Emmanuel Masonga na walikuwa wakitumia gari ya Masonga na hakuna siku Thadey aliwahi kumweleza chochote kuhusiana na mawasiliano yake na marehemu.
Alijitetea kuwa hakuwahi kumuona Thadey akizungumza na Koplo Mrisho na kwamba Thadey alikuwa miongoni mwa watuhumiwa lakini aliachiwa na tangu akamatwe, alikutana na Masonga Oktoba 2, 2020 alipomtembelea gerezani.
Fulana zilizokamatwa ni mpya
Sanga alisema upekuzi uliofanywa nyumbani kwake ulifanywa na ofisa aitwaye Malongo na sio Koplo Angelo kama Mahakama ilivyoelezwa na katika upekuzi huo, polisi walichukua fulana mbili mpya za Chadema.
Kulingana na shahidi huyo, hakushuhudia sampuli za DNA zikichukuliwa kutoka kwenye mwili wa marehemu na kusisitiza hakuna sampuli za DNA zilichukuliwa kwake na wala hakupewa haki za kisheria kama Mahakama ilivyoelezwa.
Sanga alijitetea kuwa hakuruhusiwa kuwasiliana na wakili wake wakati wa upekuzi nyumbani kwake na wala si kweli kwamba aliwaambia polisi kulikuwa hakuna haja ya kuwapekua kwanza, kabla ya upekuzi kuanza.
Alikanusha kuwaongoza polisi hadi eneo la tukio ili kuchora ramani ya eneo hilo kama polisi walivyotoa ushahidi wao na kwamba ramani hiyo aliisaini Septemba 30, 2020 siku alipokuwa anapelekwa mahakamani bila kufahamu ni nini.
Kabla ya kuanza upekuzi, Sanga aliomba awasiliane na wakili wake lakini RCO alikataa na kabla ya upekuzi kuanza, polisi walihitaji funguo za gari la mshitakiwa wa kwanza kwa maelezo wanataka kuangalia kama lina mafuta.
Ofisa wa Polisi Mrisho ndiye alichukua funguo na kwenda nje ya geti ambako gari lilikuwa limeegeshwa na walipolipekua, walikuta mkanda wa suruali na waliuchukua na kuwataka kusaini nyaraka zilizokuwa hazijajazwa kitu.
Shahidi wa pili wa utetezi, Goodluck Mbembati, alisema yeye alikuwa akiishi na mshitakiwa wa kwanza na ndugu zake wengine na Septemba 19,2020 aliondoka na gari ya mshitakiwa wa kwanza.
Mbembati alidai kuwa alilirejesha gari hilo mchana wa Septemba 26, 2020 na kwamba mshitakiwa wa kwanza alikuwa akitumia gari la Emmanuel Masonga na kwamba wakati upekuzi unafanyika kwa Sanga alikuwepo.
Usikose kufuatilia mfululizo wa simulizi hii kesho