Mbeya. Halmashauri ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, imeanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa stendi ya kisasa yenye uwezo wa kuchukua mabasi 100 kwa siku na vibanda 300 vya biashara.
Mradi huo unakadiriwa kugharimu zaidi ya Sh2.5 bilioni na utakamilika Septemba mwakani.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu, Januari 6, 2025, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chunya, Bosco Mwanginde amesema uwekezaji huo unalenga kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi na kuhakikisha usafiri wa abiria ndani na nje ya wilaya unakuwa wa uhakika.
“Januari 4, 2025, wajumbe wa kamati ya fedha walifanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi ambayo kwa sasa iko hatua nzuri za ujenzi wa miundombinu ya jengo la utawala na maeneo ya taasisi za kifedha,” amesema Mwanginde.
Amesema ujenzi huo ukikamilika utakuwa suluhisho la uhakika wa safari kwa wananchi na kufungua fursa za kiuchumi kupitia uwekezaji wa vibanda 300 vya biashara.
“Kwa sasa utekelezaji umefikia asilimia 13. Pia tunatarajia kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo maarufu machinga, ili kupanga bidhaa zao katika mazingira rasmi,” amesema mwenyekiti huyo.
Aidha, Mwanginde amesema wamebaini changamoto katika baadhi ya miradi, ikiwemo kutotekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa na dalili za ubadhirifu wa vifaa kama saruji. Hivyo, amesisitiza kuwa maelekezo yameshatolewa kwa wasimamizi kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa.
“Hatufumbii macho uzembe unaokwamisha miradi ya maendeleo, hasa ile inayotegemea nguvu za wananchi,” ameonya.
Kwa upande wake, Diwani wa Matundasi, Kimo Choga amesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua dhidi ya watu wanaokwamisha miradi hiyo ya maendeleo.
“Ni muhimu kuitisha mikutano ya wazi na kuhakikisha wasimamizi wa miradi wanawajibika, ili miradi ikamilike kwa wakati. Huu si wakati wa kuchekeana, wazembe wawajibishwe,” amesema Choga.
Naye, Diwani wa Lualaje, Tusalim Mwaijande amesema baadhi ya miradi ina changamoto ambazo tayari wamezitolea maelekezo ya kufanyiwa marekebisho.
“Tumetembelea mradi wa stendi ya mabasi na tumeona maendeleo mazuri ya ujenzi wake wa miundombinu, hususan jengo la utawala. Tuna uhakika mradi utakamilika ndani ya muda uliopangwa,” amesema Mwaijande.
Mkazi wa Chalangwa, Laston Ndomba amesema uwekezaji huo unatarajiwa kufungua fursa za kiuchumi wilayani Chunya kwa kuunganisha mikoa mbalimbali nchini.
“Tunapongeza uongozi wa halmashauri kwa kuwekeza kwenye stendi ya kisasa inayolingana na mahitaji ya kiuchumi ya wilaya yetu,” amesema Ndomba.
Mjasiriamali wa mitumba, Sekela Joel ameiomba Serikali kuharakisha ujenzi huo ili kuwaondolea wafanyabiashara changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta wateja.
“Kama vibanda hivi 300 vitakamilika, wateja sasa watajua wapi wakanunue bidhaa, na sisi wafanyabiashara tutapata nafuu ya kuwapata wengi kwa sababu lazima watakuja huku,” amesema Joel.