SHAGEMBE: Mchimba madini aliyemzima kiboko ya Kiduku

FRANK Shagembe  siyo jina kubwa ukitaja majina makubwa katika mchezo wa ngumi za kulipwa nchini lakini kwa sasa heshima yake imekuwa ikisumbua vichwa vya mabondia wakubwa.

Shagembe kijana wa miaka 24 ambaye ametoka kwenye maisha magumu akiwa mzururaji wa uchimbaji wa madini ya dhababu kule Chunya mkoani Mbeya ndiye aliyeweza kumzima Asemahle Wellem ‘Predator’ kijana kutoka Afrika Kusini  aliyepata umaarufu nchini kwa kumpiga Twaha Kiduku na kutoka sare na Selemani Kidunda.

Baada ya kufanya vizuri kwenye mapambano hayo, ilionekana kama Wellem ameshindikana ndani ya ardhi ya Tanzania na jina lake likawa maarufu vinywani mwa wapenzi wa mchezo wa masumbwi.

 Kuanzia hapo hakuna Mtanzania aliyejitokeza kwa nia ya wazi ya kutaka kupanda ulingoni Wellem ili kumaliza utawala wake zaidi ya wengi kusema wapo tayari kwa kutaja mamilioni ya shilingi.

Wengi walikuwa na shauku ya kuona nani ambaye atamaliza ubabe wa Wellem kwa mabondi wa Kitanzania hasa ukizingatia alitembeza kichapo kwa staa wa nchi, Twaha Kiduku na Selemani Kidunda alijitahidi kupata nae sare kwenye pambano lao.

Novemba 16, mwaka jana bondia Pius Mpenda, akajitokeza  kuomba kupanda ulingoni na Wellem baada ya kukutana naye Tanga katika pambano la Ngumi ya Tanga ambalo liliandaliwa na Mafia Boxing  Promotion hata hivyo inadaiwa Mpenda akaingia mitini kwa kuomba ofa kubwa.

Kutokana na hali hiyo, Mafia Boxing Promotion ikatoa jukumu hilo kwa kijana bondia wake Frank Shagembe kupanda ulingoni kumalizana na Asemahle Wellem ambapo hakuna aliyetoa nafasi ya ushindi wowote kwa Shagembe katika pambano la Knockout ya Mama ambalo lilipigwa Desemba 26, kwenye Ukumbi wa Super Dome huku Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa akiwa mgeni rasmi wa pambano hilo.

Shagembe hakupewa nafasi kutokana na kuwa na rekodi ya kucheza mapambano manne pekee ambapo pambano lake la kwanza alipanda ulingoni Juni mwaka jana dhidi ya Alibaba Tarimo ambaye alimchapa kwa Technical Knockout ya raundi ya kwanza katika pambano la raundi sita.

Lakini Agosti, mwaka jana Shagembe akamchapa bondia mwingine mzoefu kutoka Tanga, Jacob Maganga kisha Oktoba akamchakaza Muangola, Henriques Lando kwa pointi halafu Novemba akampiga tena  Stephen Ackon wa Ghana kwa Technical Knockout ya raundi ya tatu katika pambano la raundi nane.

Desemba 26, mwaka jana Shagembe akaumaliza mwaka vizuri kwa kufanikiwa kumchapa kiboko wa Twaha Kiduku kwa pointi katika pambano Knockout ya Mama ambalo lilipigwa kwa raundi nane huku likiwa limehudhuriwa  waziri mkuu.

Ni matokeo ambayo yamewashangaza wengi kwa vile Wellem ni miongoni mwa mabondio wazuri nchini Afrika Kusini na alionekana kama ameshindikana hapa Tanzania.

Mpaka sasa Shagembe ameshinda  mapambano yake yote manne kati ya hayo mawili ameshinda kwa Knockout  huku akiwa bondia wa tatu katika mabondia 31 wa uzani wa super middle wakati duniani akiwa 145 katika mabondia 1717 wa uzani huo.

Spoti Mikiki limefanya mahojiano na Shagembe aliyeitoa nchi kimasomaso dhidi ya Wellem ambapo amefichua mambo kadhaa kuhusu maisha yake na ngumi kiujumla hadi alipotikisa mwishoni mwa  mwaka jana.

Shagembe mwenye hadhi ya nyota mbili anaeleza kuwa mchezo wa ngumi kwake ameanza kupenda tangu akiwa mtoto kwao Mbeya kabla kutafuta kwa kutokea.

“Binafsi mchezo huu nimeanza kupenda zamani tangu wakati nipo Mbeya na kwa bahati mbaya sana sijawahi kupita kucheza ngumi za ridhaa kama mabondia wengine,” anasema bondia huyo.

“Kiukweli wakati nipo Mbeya kuna mtu anaitwa Mabula Ndugula yeye ni mtu wa Mwanza lakini  yupo Mbeya kwa ajili ya kutafuta hivyo nimekutana naye kwenye masuala ya mambo ya uchimbaji wa madini, Chunya.

“Naweza sema yeye amenilea wakati nipo Mbeya na ndiye ambaye aliniunganisha na Salim Mtango ambaye naye alinipeleka kwa kocha Hamisi Mwakinyo yaani nilitoka Mbeya hadi Dar halafu nikaenda Tanga,” anasema Shagembe

Nani sababu ya kupenda ngumi?

“Mtu ambaye amefanya nipende mchezo huu kwangu ni Anthony Joshua na ndiye bondia wangu ambaye nimekuwa nikijifunza kupitia yeye na wakati wote amekuwa kioo cha kuendelea kufanya mazoezi kwa bidii  ili kufikia ndoto zangu.”

Wakati unaambiwa utapigana na Asemahle Wellem kwako hali ilikuaje?

“Kwanza nilikuwa na hofu kutokana na ubora na ukubwa wake lakini upande mwengine nikajipa matumaini ya kuweza kumpiga ingawa sehemu kubwa ya watu wengine walitegemea kuona napigwa kutokana na kile ambacho Wellem alishakifanya hapa kwetu kwa mabondia wengine.

“Unajua hata baadhi ya mabondia wengine ambao nipo nao gym moja hakuna ambaye alitegemea kuona naweza kushinda zaidi wengi waliamini kwamba ningetoa ushindani lakini kilichotokea kimewashangaza wengi kwa sababu hawakutegemea.

“Kitu ambacho wengi hawakijui ni kwamba nilikuwa nafanya mazoezi sana na niliamini naweza kushinda sikutaka kuogopa jina lake, nashukuru uongozi wangu wa Mafia Boxing Gym kwa sababu uliweza kunisimamia vizuri wakati wa maandalizi na nimeweza kushinda.

“Lakini siwezi kumsahau mama yangu kwa sababu alifunga siku mbili ili mtoto wake nishinde na imekuwa faraja kwa familia yangu kwa sababu nilimwambia kwamba pambano hili limeshika hatima ya maisha yangu kwenye mchezo huu,” anasema Shagembe.

Uongozi umepanga kukuzawadia gari, ulitegemea?

“Hapana, sikutegemea kwa sababu gari zilizotoka katika pambano la Knockout ya Mama ilikuwa ni wale ambao walifanikiwa kushinda kwa Knockout lakini sasa imekuwa ‘surprise’ kubwa kwangu, najua nilikuwa najua nitamiliki gari ila siyo kwa sasa imekuja haraka.”

Nini unawaambia Kiduku na Kidunda?

“Kwanza hao ni kaka zangu sina cha kusema zaidi ya kuwapa heshima yao haijalishi nini kilitokea kwao na siwezi kusema nataka kupigana nao moja kwa moja ila kama itatokea kwa uongozi kubariki basi kazi itafanyika,” anasema Shagembe.

Shagembe alisema atajitahidi kufanya mazoezi ili awe bora zaidi.

Related Posts