Ujerumani. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Nancy Faeser ametangaza kuwaondolea kinga ya uhamiaji raia wa Syria wanaoishi na kufanya shughuli mbalimbali nchini humo.
Takriban raia 975,000 wa Syria wanaishi na kufanya shughuli mbalimbali nchini Ujerumani, ikiwemo kuajiriwa kwa kile ambacho Nancy anadai walikuwa wakitumia kigezo cha kutetereka kwa amani nchini mwao.
Tovuti ya Russia Today ikinukuu Kituo cha Funke cha nchini Ujerumani, imeripoti kuwa uamuzi huo wa Ujerumani umefikiwa baada ya hali ya kiusalama na kiutawala kutengemaa nchini Syria, hivyo kutoa fursa kwao kuwarejesha wahamiaji hao.
Akizungumza katika mahojiano na Kituo cha Funke cha nchini Ujerumani, jana Jumapili, Januari 5, 2025, Nancy amependekeza raia wa Syria wanaoishi Ujerumani kuanza kurejea nchini kwao.
Pendekezo hilo linakuja ukiwa umepita mwezi mmoja tangu kundi la Hayat Tahrir al-Sham litangaze kuuangusha utawala wa aliyekuwa Rais wa taifa hilo, Bashar al-Assad.
Uvamizi huo dhidi ya vikosi vya Serikali ulisababisha kukomeshwa kwa utawala wa familia ya Assad, ulioitawala Syria kwa zaidi ya miaka 50. Kabla ya Bashar, taifa hilo liliongozwa na baba yake mzazi, Hafez al-Assad.
Nancy amebainisha njia tatu zitakazotumika kuamua iwapo raia wa Syria anayeishi nchini humo atabakia ama kuondelewa, kuwa ni pamoja na raia wenye mchango na wanaotumikia jamii ya Ujerumani watapewa fursa ya kubaki.
Pia, amesema wanaohitaji kurejea kwa hiari yao, Ujerumani itawawezesha kufanya hivyo huku wanaoshtakiwa ama wenye historia ya kufanya makosa ya jinai wakirejeshwa nchini humo kwa mujibu wa sheria ‘Deportation.”
“Sheria zetu zinaeleza wazi, Ofisi ya Usimamizi na Uratibu wa Wahamiaji (BAMF) itaanza kupitia na kuwaondolea kinga wahamiaji wote kutoka Syria, hususan wale ambao hawahitajiki kuwekewa kinga hii kwa sababu hali imeshatengemaa nchini kwao,” amenukuliwa Nancy na gazeti la Der Spiegel.
Waziri huyo ameenda mbali zaidi akisema kinga hiyo itaachwa kwa wale wenye kibali maalumu cha kufanya kazi ama kusoma nchini Ujerumani. Wengine watatakiwa kurejea nchini kwao.
Nancy amesisitiza kuwa raia wa Syria wanaofanya kazi nchini Ujerumani wanapaswa kulindwa na wale wanaotaka kurejea wasaidiwe, huku akidokeza kuwa wenye historia ya uhalifu watarejeshwa haraka iwezekanavyo.
“Tayari tumekamilisha utaratibu wa kisheria wa kusimamia na kuratibu suala hili na tunaanza utekelezaji wake haraka iwezekanavyo,” ameongeza.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock alisafiri hadi nchini Syria wiki iliyopita na kufanya mazungumzo na kiongozi wa taifa hilo, Ahmed al- Sharaa maarufu Abu Mohammad al-Julani kuhusiana na masuala mbalimbali, ikiwemo ya kisiasa.
Miongoni mwa mambo waliyojadiliana ni pamoja kuitaka Syria mpya kuimarisha kwa mifumo ya kisiasa, kiutawala, haki za binadamu na usawa ili kuiwezesha kuondolewa vikwazo vya kiuchumi vinavyolikumba taifa hilo.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika.