Waganga wa jadi wapigwa marufuku kung’ang’ania wagonjwa

Shinyanga.  Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Dk Faustine Mulyutu, amewataka waganga wa jadi wakiona wagonjwa wenye dalili za maambukizi ya malaria wasiwang’ang’anie, bali wawashauri kwenda vituo vya afya.

Dk Mulyutu ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Januari 6, 2025, wakati wa uzunduzi wa kampeni ya ugawaji vyandarua kwa wananchi iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa, ikiongozwa na Wizara ya Afya na Tamisemi.

“Watu wa tiba asilia (waganga wa jadi) wenyewe pia ni wenzetu kwa sababu wanatusaidia kutibu wagonjwa, lakini endapo wataona wagonjwa hao wana dalili za maambukizi ya ugonjwa wa malaria wasiwang’ang’anie, bali wawashauri kufika kwenye vituo vya afya kwa matibabu zaidi,” amesema Dk Mulyutu.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa tiba asilia Mkoa wa Shinyanga, Iddy Mpyalimi amesema ni waganga wachache wanaoharibu utaratibu.

“Kwa kawaida tunatoa elimu kwa wagonjwa wanaokuja kutibiwa waje na kitambulisho kinachoonyesha vipimo vimefanyika na matibabu ya awali na sisi ndipo tunapoanzia, ni waganga wachache wanaoharibu utaratibu na kutibu watu bila kutoa elimu yoyote,” amesema Mpyalimi.

Ofisa mdhibiti wa wadudu dhurifu kutoka Ofisi ya Raisi- Tamisemi, Best Yoram, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha asilimia 80 ya kaya nchini zinajiandikisha kupata vyandarua vyenye dawa vinavyotolewa bila malipo, ili kukabiliana na ugonjwa wa malaria.

“Kupitia kampeni hii ya kupokea vyandarua, Serikali imejipanga kuhakikisha asilimia 80 ya kaya za Watanzania zinajiandikisha ili kupata vyandarua vyenye dawa vinavyotolewa bila malipo ambavyo vitasaidia kupunguza maambukizi ya malaria,” amesema Yoram.

Hatua hiyo ya wizara imekuja kutokana na taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kueleza kuwapo kwa ongezeko la maambukizi kutoka milioni 249 hadi milioni 263 kwa kipindi cha mwaka 2022 hadi 2023.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa vifo vimepungua kutoka 608,000 (2023) hadi 597,000 (2024), huku asilimia 95 ya maambukizi yakionyesha yapo barani Afrika ikiongozwa na Nigeria, DRC, Uganda, Ethiopia, Msumbiji na Tanzania.

Ofisa kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Makaria, Peter Gitanya amesema Shinyanga maambukizi yapo juu hadi kufikia nafasi ya nne kitaifa ambayo ina asilimia 16, ikiongozwa na Tabora yenye asilimia 23, Mtwara asilimia 20, Kagera asilimia 18, Shinyanga asilimia 16 na Mara asilimia 15.

“Waandishi wa habari muwe chachu ya kutoa elimu kwa wananchi kupitia habari, ili kuepukana na mila potofu juu ya vyandarua vinavyotolewa bila malipo kwamba vinaleta kunguni na wengine kudai zinapunguza nguvu za kiume,” amesema.

Related Posts