Hii leo,Jumatatu, waziri wa mambo ya nje Assad al Shaibani pamoja na waziri wa ulinzi na mkuu wa ujasusi wa nchi hiyo, wamewasili Umoja wa Falme za kiarabu katika ziara yao ya kwanza nchini humo tangu waasi walipouondowa utawala wa Bashar al- Assad.
Waziri mpya wa mambo ya nje wa Syria Assad al Shaibani ameandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X ulioandama na picha inayomuonesha amewasili Umoja wa Falme za Kiarabu akiandamana na waziri wa ulinzi Murhaf Abu Qasra na mkuu wa ujasusi Anas Khattab. Amesema anatarajia kutengeneza mahusiano mazuri na nchi hiyo ya Umoja wa Falme za Kiarabu.
Wasiwasi wa UAE
Wachambuzi wanasema Umoja wa Falme za Kiarabu,UAE ina mashaka makubwa na viongozi wapya wa Syria, ikionesha kutoamini siasa za mwelekeo wa kidini na kukhofia kuongezeka kwa ushawishi wa Uturuki katika nchi hiyo iliyoshuhudia vita.
Ziara hii pia imekuja baada ya hapo jana viongozi hao wa Syria kuitembelea Qatar, na wiki iliyopita Saudi Arabia. Qatar na Uturuki ambazo ziliwaunga mkono waasi waliompinga Bashar Al Assad zimekwisha fungua balozi zao mjini Damascus mara Assad alipokimbilia mjini Moscow,Urusi.Soma pia: Watu zaidi ya 100 wauawa kaskazini mwa Syria
Waziri wa mambo ya nje wa mpito wa Syria Assad al Shaiban akiwa Doha hapo jana alisisitiza kwamba dhamira kubwa ya utawala mpya ni kuijenga upya nchi yao na kurekebisha mahusiano na mataifa ya kiarabu na ya kigeni.
“Njia tunayodhamiria kuifuata kama Syria ni kuijenga upya nchi yetu,kurudisha mahusiano na mataifa ya kiarabu na kigeni, kuwawezesha watu wa Syria kupata haki zao za kiraia na za kimsingi,pamoja na kuiwakilisha serikali ambayo wasyria watahisi kuwakilishwa kwa ujumla wao.”
Mshauri wa rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Anwar Gargash mnamo mwezi uliopita alisikika akisema kwamba,UAE ina mashaka makubwa na mitizamo ya itikadi kali za kiislamu kwa watawala wapya wa Syria.
Marekani yalegeza vikwazo kwa Syria
Wakati huohuo Marekani inajiandaa kutangaza kulegeza vikwazo vinavyohusiana na kuipatia msaada wa kibinadamu na huduma nyingine za msingi kama umeme,Syria huku lakini ikiendeleza vikwazo vilivyowekwa dhidi ya utawala wa nchi hiyo.
Uwamuzi huo wa kulegeza vikwazo wa serikali inayomaliza muda wake ya rais Joe Biden utatuma ujumbe wa nia njema kwa watawala wapya nchini Syria na unalenga kufungua njia ya kuimarisha hali ya maisha katika taifa hilo lakini pia kuubakisha ushawishi wa Marekani.
Ripoti zinasema kwamba rais Joe Biden alisaini hatua hiyo mwishoni mwa juma ambapo idara ya fedha imeleekezwa kuyaruhusu mashirika ya msaada na makampuni ya kutoa huduma za msingi kama maji, umeme na misaada mingine ya kibinadamu kuisaidia Syria.
Wakati huohuo waziri wa mambo ya nje Antony Blinken wiki hii atakutana na wenzake katika Umoja wa Ulaya, mjini Roma Italia kuijadili Syria, wakati mataifa hayo ya Magharibi yakijiandaa kuwa na ushirikiano na utawala mpya wa Syria unaoongozwa na wenye misimamo mikali ya kiislamu.