Anwani za makazi milioni 12.8 zafikiwa nchini

Arusha. Serikali imefanikiwa kutambua na kuhakiki taarifa za anwani za makazi milioni 12.8 na kuzisajili kwenye mfumo wa kidigitali wa anwani za makazi (NaPA).

Taarifa hizi zinalenga kujenga msingi madhubuti wa utoaji wa huduma za mawasiliano, huduma za Serikali kwa wananchi na utekelezaji wa shughuli za kijamii, kiuchumi na kiutawala.

Akizungumza  leo Jumanne Januari 7, 2025 mkoani Arusha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohamed Abdulla  amesema hadi sasa jumla ya taarifa za anwani za makazi 12,823,983 zimekusanywa na kuingizwa kwenye mfumo wa kiserikali.

Abdulla aliyewakilishwa na mkurugenzi wa ufuatiliaji na tathmini wa wizara hiyo, Elisa Mbise amesema katika awamu ya kwanza, walifanikiwa kukusanya taarifa za anwani za makazi milioni 12.3 na awamu ya pili, iliyoanza mwaka jana, imekusanya taarifa 523,983.

“Hadi sasa tumefikia halmashauri 35 nchini na tunatarajia kufikia Juni mwaka huu kukamilisha awamu hii,” amesema Abdulla.

“Wengi hujiuliza kwa nini tunafanya uhuishaji wa taarifa kila mwaka, lakini hii inatokana na ongezeko la makazi na mitaa mipya ambayo nayo inahitaji huduma kama zile zilizosajiliwa.”

Amesema mfumo huo, mbali na kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali, pia utachangia kukuza uchumi wa kidigitali kupitia biashara za mtandaoni, hususan zile zinazovuka mipaka ya nchi.

Mradi wa anwani za makazi unatekelezwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mradi huo pia, unaelezewa kwamba unakwenda kusaidia kubaini mahitaji ya dharura ya wananchi na kurahisisha huduma za haraka wakati wa majanga.

“Niwaondoe hofu wananchi kuwa mfumo huu wa anwani za makazi unazingatia viwango vya kimataifa vilivyowekwa na Umoja wa Posta Ulimwenguni (UPU), Umoja wa Posta wa Pan-African (PAPU) na mashirika mengine ya kimataifa kama Shirika la Viwango vya Kimataifa (ISO),” amesema Abdulla.

Katika ufunguzi wa semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Amri Mkalipa amewataka wenyeviti na watendaji wa mitaa na vitongoji kuzingatia haki na wajibu wao ili kuhakikisha kazi hiyo inafanikiwa.

Mkalipa amesema mafunzo hayo ya siku mbili yatasaidia kurahisisha utekelezaji wa kazi ya ukusanyaji taarifa zitakazofanyika kwa siku 10 kuanzia Januari 9-19, 2025, katika mitaa na vitongoji vyote vya Halmashauri ya Meru.

Aidha, amewaonya wananchi, viongozi wa kisiasa na Serikali watakaojaribu kukwamisha utekelezwaji wa kazi hiyo, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.

“Wale watakaotaka kukwamisha zoezi hili, viongozi wangu hakikisheni mnachukua hatua za kisheria dhidi yao. Ofisi yangu itakuwa tayari kushirikiana nanyi,” amesema Mkalipa.

Related Posts