Dar es Salaam. Wakati minyukano ya wazi na ya chini kwa chini ikiendelea kuelekea uchaguzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ngazi ya taifa, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika ametoa onyo kwa wanachama, wagombea na mawakala wao, akiwataka kufuata miongozo ya kampeni la sivyo hatua zitachukuliwa dhidi yao.
Miongozo hiyo ni ile iliyotungwa na kuanza kutumika mwaka 2012, kuhusu taratibu za kuendesha kampeni na kujitojihusisha na vitendo vya rushwa.
Amesema kwa yeyote atakayeona kuna mwanachama au mgombea anayekiuka miongozo hiyo, awasilishe malalamiko rasmi kwenye ofisi yake au kwa mamlaka zinazohusika kulingana na anayetuhumiwa, ili hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa haraka.
Pamoja na suala hilo, Mnyika amewatangazia wagombea, wapambe na wanachama wa chama hicho, kuwa uchaguzi huo utakuwa huru na wenye uwazi wa kutosha.
Mnyika amesema hayo kipindi ambacho dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu kuwania nafasi mbalimbali ngazi ya taifa ya chama na mabaraza likiwa limefungwa huku kukishuhudiwa mmtifuano baina ya wagombea na wapambe wao.
Mchuano mkali unaosababisha tishio kwa uimara wa chama ni wa nafasi ya uenyekiti, unakutanisha mafahari wawili – Mwenyekiti Freeman Mbowe anayetetea nafasi hiyo na Makamu wake-Bara, Tundu Lissu.
Wagombea hao ambao kampeni zao zimezua gumzo, pia wanashindana na Romanus Mapunda na Charles Odero, ambao hata hivyo hawatajwi sana.
Mbali na hao, mchuano pia unatarajiwa baina ya wajumbe wa kamati kuu, John Heche na Ezekiel Wenje ambaye pia ni mwenyekiti wa Kanda ya Victoria kwenye kinyang’anyiro cha umakamu mwenyekiti-Bara.
Wawili hawa wamejitanabaisha kuwaunga mafahari wawili wanaopigania uenyekiti. Heche anamuunga mkono Lissu huku Wenje akiwa upande wa Mbowe.
Katikati ya mvutano huo uliosababisha kambi hizo kurudiana na Maneno na tuhuma mbalimbali, leo Jumanne, Januari 7, 2025, Mnyika amekutana na wanahabari makao makuu ya chama hicho, Mikocheni jijini Dar es Salaam na kuelezea kile kinachoendelea baada ya dirisha la kufungwa na maandalizi ya mkutano mkuu wa Januari 21, 2025, utakaofanyika Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Mbali na hilo, Mnyika amesema katika kipindi cha uchukuaji na urejeshaji fomu kuna tuhuma za viongozi kuvunja miongozo ya chama, licha ya kwamba alikwishatoa tahadhari wakati wa ufunguzi wa dirisha hilo.
“Nitumie fursa hii kusisitiza na safari hii iwapo kuna kiongozi au mwanachama au mgombea atakayeona yeyote anakiuka miongozo hiyo, aweze kuwasilisha rasmi kwa katibu mkuu wa chama au kwa mamlaka zingine ili kudhibiti hali hiyo,” amesema Mnyika.
Katika maelezo yake, Mnyika amesema katika kipindi hiki, baada ya wagombea kurejesha fomu, anajua kampeni zitakuwa kubwa, hivyo mgombea na wakala wake hawataruhusiwa kufanya kampeni kabla ya muda kutangazwa.
“Mgombea au kampeni meneja wake hataruhusiwa kumkashifu mgombea mwenzake kwa kusambaza nyaraka, vipeperushi au kutoa taarifa kwa njia ya mitandao ya kijamii, zisizohusiana na wasifu wake,” amesema.
Mnyika amesema itakuwa marufuku kusambaza taarifa zenye lengo la kudharau na kukashifu kiongozi yeyote wa chama hicho.
“Ni marufuku mgombea au wakala wake kufanya kampeni kwa kuhusisha ukanda, udini, ukabila au ubaguzi wa aina yeyote ile na mgombea au wakala lazima azingatie muongozo wa rushwa,” amesema.
Mnyika amesema iwapo itabainika mwanachama amevunja muongozo huo, kwanza atachukuliwa hatua ya kupewa onyo mara mbili na iwapo itathibitika ataondolewa kwenye mchakato wa uchaguzi.
“Pia atafungiwa kugombea nafasi yeyote ndani ya chama kwa muda utakaoamuliwa na mamlaka husika, isipokuwa muda huo hautazidi miaka mitano,” amesema Mnyika.
Kuhusu rushwa, Mnyika amesema ni marufuku kwa mgombea kutoa vinywaji, chakula au zawadi nyinginezo kwa wajumbe na wapiga kura kwa lengo la kujipatia kura.
“Pia haitakiwi kuwasafirisha wajumbe kuhudhuria mkutano kwa ngazi husika kwa ajili ya uchaguzi, kwa lengo la kujipatia kura lakini pia haitakiwi kutoa ahadi kwa wapiga kura,” amesema.
Onyo hilo la Mnyika limewaibua wadau wa uchaguzi huo, akiwemo Odero anayewanai uenyekiti ambaye amesema: ”Nasikitika kwamba Katibu Mkuu Mnyika amechelewa kuzungumzia hilo, lakini pia amechelewa kuchukua hatua, jambo ambalo kwa maono yangu limechangia kuleta makovu na madhara makubwa ndani ya chama.”
“Najiuliza hivi mtindo wa viongozi wa wilaya, mkoa, kanda kujitokeza hadharani na kuanza kusema tunampigia kura mgombea fulani, je, Mnyika ameliona? Je, ameanza kulifanyia kazi?” amehoji.
Odero amesema: “Na ninadhani kama katibu mkuu yupo ‘serious’ aanze kuandika barua kali ya onyo kwa Lissu na Mbowe kwa kuvunja maadili ya chama, kuhusu namna ya kufanya kampeni. Mfano Lissu wakati anatangaza nia alikuwa na wapiga kura, kadhalika Mbowe kwa kitendo cha kukusanya wapiga kura nyumbani kwake na kumsindikiza kuchukua fomu.”
Kwa upande wake Yericco Nyerere, mjumbe wa mkutano mkuu anayemuunga mkono Mbowe, pia amesema “onyo la katibu mkuu limechelewa kutolewa wakati sehemu ya wagombea wamekwisha kuwaumiza wenzao, limetoka wakati mmoja wa wagombea amekwisha kuwaumiza wagombea wenzake.
“Tufanye kampeni kwa kufuata miongozo ya chama bila kutukanana na au kuchafuana. Mfano, mimi nimeeleza kwa hoja kwa nini ninamuunga mkono Mbowe na simuungi mkono Lissu, sasa ninaiomba ofisi ya katibu mkuu isimamie kuhakikisha matusi dhidi ya viongozi yanadhibitiwa,” amesema.
Naye Gervas Lyenda, mmoja wa mameneja kampeni wa timu Lissu amemuunga mkono Mnyika, akisema wao upande wa Lissu wameendelea kuiishi miongozi hiyo na kuwasihi wote kufanya hivyo kwa kuwatunzia heshima na hadhia viongozi wakuu – Lissu na Mbowe.
“Tunaiheshimu (miongozo) na tuko makini nayo na tunaifuata na ndiyo maana huwezi kuona mtu anayemuunga mkono Lissu anamshambulia Mbowe au akimshushia heshima, sisi tunajikita kwenye hoja na vipaumbele vyetu,” amesema.
“Nawashauri wote tunaomuunga mkono Lissu, kuendelea kuwatunzia heshima Mbowe na Lissu, hawa wote ni wagombea, wanachama na chama hiki kinapaswa kuendelea baada ya uchaguzi.
“Tusije kuumizana sasa na kutengenezeana vidonda vitakavyochukua muda kupona, huu ni mwaka wa uchaguzi, tunapaswa kuwa na uchaguzi mzuri wa ndani ili tuwe na muda mfupi wa kuwekana sawa,” amesema Lyenda.
Katika mkutano huo, Mnyika ambaye ni msimamizi mkuu wa uchaguzi ndani ya chama hicho, amesema jumla ya wagombea 300 wamejitokeza kwa ngazi mabaraza na kwa ngazi ya taifa ambako watia nia ni 56. Wagombea wote watasailiwa na Kamati Kuu kuanzia Januari 10, 2025.
“Upande wa Baraza la Wazee wagombea ni 85, Bawacha 93 na Bavicha 66…Hawa ni wagombea wengi na mchakato wa kuwasaili na uteuzi unahusu vikao vya kamati kuu vitakavyoanza Januari 10 mwaka huu kwa wagombea wa Bavicha na Bazecha na Januari 11 kwa upande wa Bawacha.
“Kazi ya usaili itaendelea Januari 19, mwaka huu upande wa chama na wakati huo kamati kuu itafanya kazi ya kuandaa mkutano mkuu na Baraza kuu wa chama na itaanza kukutana Januari 18,” amesema Mnyika.