Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango leo Jumanne, Januari 7, 2025 amehudhuria kuapishwa kwa Rais mteule wa Ghana, John Dramani Mahama uliofanyika katika Uwanja wa Independence Square jijini Accra nchini Ghana.
Dk Mpango amepata muda wa kumpongeza Rais Mahama baada ya kuapishwa akichukua nafasi ya Nana Addo Akufo-Addo aliyemaliza muda wake.
Rais Mahama alikuwa kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo, alishinda urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika Desemba 7, 2024 na aliwahi kuwa rais wa nchi hiyo katika muhula wa mwaka 2012 hadi 2017.
Kiongozi huyo aliyepeperusha Chama cha National Democratic Congress (NDC) alimshinda makamu wa rais wa nchi hiyo, Mahamudu Bawumia aliyekuwa akiwakilisha chama tawala cha New Patriotic Party (NPP).