Kilombero. Wakazi wa Kata ya Mlabani Halmashauri ya Mji wa Ifakara, wilayani Kilombero, wameipongeza Serikali kwa kutenga fedha na hatimaye kuchonga barabara mpya zitakazounganisha mitaa yao.
Baadhi ya wananchi hao, akiwamo Elias Selemani akizungumza wakati kazi ya uchongaji barabara hizo ikiendelea amesema ujenzi wa barabara hizo utaboresha mawasiliano na kurahisisha usafiri hasa katika kipindi hiki ambacho mvua zimeanza kunyesha.
Selemani amesema kutokana na jitihada hizo, hata michango wanayochangishwa ya fedha kwa ajili ya kutengeneza makaravati katika maeneo yanayohitajika ili kuboresha zaidi miundombinu hiyo, wataitoa bila kinyongo.
Diwani wa Mlabani, Ladislaus Mloti amempongeza mbunge wa Kilombero, Abubakary Asenga kwa juhudi zake za kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo. “Matengenezo haya yamekuja wakati muafaka, maeneo mengi ya kata hii yanauhitaji mkubwa wa barabara kutokana na ukuaji wa kasi wa mji wa Ifakara na ongezeko la idadi ya watu, uamuzi wa mbunge kuingiza fedha za Mfuko wa Jimbo kwenye ujenzi huu, unapaswa kupongezwa,” amesema diwani huyo.
Amesema jumla ya Sh25 milioni zimetumika kuchonga barabara za mitaa ya Kata ya Mlabani, lengo likiwa ni kuzifanya zipitike kirahisi hasa wakati wa mvua.
Mloti amesema tayari kilomita tatu za barabara zimechongwa ndani ya siku mbili huku akisisitiza barabara hizo zitasaidia kufungua njia za kuelekea mashambani.
Amesema mvua iliyonyesha mwaka jana iliharibu barabara nyingi, hivyo kusababisha changamoto kubwa ya usafiri.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Muungano, Peter Utyatya amesema maeneo yote yenye changamoto yatashughulikiwa ili kuhakikisha barabara zinapitika msimu mzima.
Mbunge wa Kilombero, Asenga amesema kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara za mitaa kutawasaidia wananchi kusafiri kwa urahisi kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na maendeleo ya kijamii.
“Tunatambua adha kubwa wanayokumbana nayo wananchi, ndiyo maana nimeona ni vizuri tukatumia fedha hizi za Mfuko wa Jimbo safari hii zijenge hizi barabara,” amesema Asenga.