Gambo: Mimi mbunge nina vikao vya Bunge

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kudai mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo haudhurii vikao, mbunge huyo amesema suala hilo linahitaji elimu kwa sababu yeye ni mbunge na ana vikao vya Bunge.

“Mimi sio ofisa tarafa, siyo mtendaji wa mtaa wala kata, mimi ni mbunge wa wananchi ambaye kazi yangu kubwa kwenda kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania kuwawakilisha wananchi wa Arusha Mjini.

“Katika Bunge yeye sio mjumbe, sasa anaposema sihudhurii vikao anamaanisha nini? Anatakiwa afafanue, maana kumuongelea mjumbe hupaswi kuongea jumla jumla tu,” amesema Gambo.

Jana, Jumatatu Januari 6, 2025 wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega aliyekuwa akikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Mianzini- Olemringaringa- Sambasha- Tumbolo ya kilomita 18 kwa thamani ya Sh23 bilioni, Makonda alidai Gambo haudhurii vikao.

Makonda alisema hayo, baada ya Gambo kuelezea changamoto za barabara za Mkoa wa Arusha, akimuomba Ulega ampatie majibu.

“Nimefurahi kumsikia mheshimiwa Gambo ambaye hivi sasa kutamka jina la Makonda anapata tabu sana, lakini mimi ndiyo mkuu wake wa mkoa. Hata hapa amekuwa na kigugumizi, mwanzoni alikuwa anasema ananenepa kwa sababu ya Makonda, sasa kulitamka limekuwa gumu kwa sababu napiga spana mtu yeyote yule ili mambo yaende.

“Nimsaidie waziri (Ulega) hoja alizozisema Gambo kwenye vikao haji ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu kumsubiri kiongozi kwenye public (umma) ili umvizie upachike mambo,” alisema Makonda.


Makonda alivyomvaa Gambo mbele ya waziri

Makonda alisema mtu akienda kwenye vikao atapata majibu na huwezi kuwa kiongozi ukasubiri kiongozi mkubwa anayekwenda mahali fulani na wewe unakwenda na kumpachikia neno.

“Hebu fikiria kama mtani wangu (Ulega) hapa kama angekuwa hajajua vizuri si angeanza kunong’onezana na watendaji wake kwamba ilikuaje, ilikuaje. Viongozi hawa ni watu wenye heshima, njoo kwenye vikao na jenga hoja,” alisema Makonda.

 “Tumeshapewa msimamo wa Serikali barabara ile inakwenda kujengwa kwa lami na Waziri wa Ujenzi (Ulega) amesema. Sasa Gambo anataka kuja kusemea huku sasa uwe unahudhuria, mimi sipendi mtu haudhurii vikao halafu anasubiri kwenye public (umma) anaanza kumchomekea kiongozi maneno.”

“Ooh tupe leo kauli? Kauli ni kwamba nenda kwenye vikao,” alisema Makonda, huku akishangiliwa na wananchi wa Ilboru wilayani Arumeru.

Leo, Jumanne Januari 7, 2025 akihojiwa na Wasafi FM, Gambo amesema vikao vyake ni vya Bunge na kamati huku akihoji katika vikao hivyo mkuu wa mkoa anaingia kama nani.

Hata hivyo, mwandishi alimuuliza Gambo huenda vikao anavyozungumzia Makonda vinahusiana na maendeleo ambacho pia waziri alikuwepo, mbunge huyo akajibu: “Sasa mbunge ana vikao vingi, nina vikao na wananchi, nina mikutano ya hadhara ambayo sipangiwi na mkuu wa mkoa, mikutano ya ndani ya chama, hata jana tulikuwa na kikao cha halmashauri kuu ya chama ya mkoa.

“Yeye alipanga kikao chake, sasa mimi mbunge ninayetokana na wananchi, kazi yangu namba moja ni kuwa sauti ya watu. Kuna miradi tumeisemea kwa miaka mingi ambayo hadi sasa haijapata utatuzi, ndiyo ambayo jana nimemueleza Waziri wa Ujenzi mheshimiwa Ulega,” amesema Gambo.

Pia, amesema kuna mradi wa Barabara wa Arusha – Kibaya – Kongwa ambao Arusha kuna kilomita 27 zinatakiwa kujengwa njia nne kutoka kona ya Mbauda hadi inapojengwa stendi.

Gambo amesema mradi huo ukijengwa utaondoa mafuriko na kuondoa msongamano wa foleni ambao ulisainiwa mkataba tangu mwaka 2022 hadi leo mkandarasi hajaanza kazi hiyo.

“Mkuu wa mkoa siyo mwenye dhamana na Tanroads (Wakala wa Barabara Tanzania) na miradi iliyosainiwa, bali mwenye dhamana ni Waziri wa Ujenzi ndiyo maana nikamuuliza ili atupatie majibu hadharani wananchi wajue hatima ya mradi.

“Sasa majibu ya hizo hoja ndipo ikaja sijui anataja jina langu, sijui nini, ndiyo maana nikawa nacheka kwa sababu niliyemuuliza siyo yeye bali ni waziri, kwa hiyo nilikuwa nategemea majibu kwa waziri,” amesema.

Hata hivyo, Gambo amesema kama Waziri Ulega jana hakujibu hadharani basi atakutana naye bungeni na atamuuliza maswali hayo hayo hadi majibu yapatikane akisema ndiyo kazi aliyopewa na wananchi.

“Maswali kama hayo hata ningemuuliza mkuu wa mkoa ingebidi amtafute waziri amuulize kwa sababu hana bajeti, hana makandarasi, hana Tanroads. Mtu mwenye mamlaka ni waziri mwenye dhamana ya ujenzi ndiyo maana akija Rais, mbunge unapewa nafasi ya kueleza mafanikio na changamoto.

“Yeye ni nani, anayetaka watu wasitoe changamoto katika nchi hii,” amehoji Gambo aliyewahi pia kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Related Posts