Mbeya/Mpanda. Wakati baadhi ya wananchi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wakionyesha hofu, wakisita kupeleka watoto shule kutokana na mlipuko wa kipindupindu, viongozi na wataalamu wamewatoa wasiwasi.
Shule za msingi na sekondari zinatarajiwa kufunguliwa Januari 13, 2025.
Taarifa ya Desemba, 2024 ya Wizara ya Afya ilisema mikoa 23 nchini ilikumbwa na kipindupindu tangu mwaka 2023 ikiwamo Mbeya, Rukwa na Katavi. Songwe ilitajwa kwamba iliweza kuudhibiti ugonjwa huo.
Desemba 19, 2024, Jiji la Mbeya liliripotiwa kuwapo wagonjwa 46 na vifo vitatu, ikielezwa mkoa umetenga maeneo maalumu kwa ajili ya wagonjwa. Kata 18 kati 36 jini humo zilitajwa kukumbwa na ugonjwa huo.
Halmashauri tatu za Mbeya Jiji, Mbeya DC na Chunya zilitajwa kuwa na wagonjwa wa kipindupindu, wakuu wa wilaya na kamati za afya wakitakiwa kukutana haraka.
Mkoani Katavi, halmashauri za wilaya ya Mpanda na Tanganyika zimeripotiwa kuwa na wagonjwa zaidi ya 17.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa mikoa hiyo wamesema wana hofu kuhusu afya za watoto wao shule zikifunguliwa.
Munira Jamilu, mkazi wa jijini Mbeya amesema: “Hatujasikia kauli ya Serikali kama maeneo ya shuleni kuna tahadhari gani, kimsingi inatupa hofu kwa kuwa mara ya mwisho walitaja maeneo ya vyuo kuwapo ugonjwa huu.”
Mkazi mwingine, Victoria Njema amesema changamoto iliyopo ni uhaba wa majisafi akiomba Serikali iboreshe miundombinu.
“Maji ni ya visima na hatuna uhakika na usalama wake, watoto wetu hata huko shuleni hatujui hatima yao,” amesema.
Peter Daniel, amesema baadhi ya chemba za majitaka hutiririsha maji kwenye mito ambayo maji yake hutumika majumbani.
Juliana Mashaka, mkazi wa mtaa wa Nsemulwa wilayani Mpanda, mkoani Katavi amesema wana hofu kuhusu watoto kuambukizwa kipindupindu akishauri kuboreshwa miundombinu.
“Shule zetu asilimia kubwa hazina huduma ya maji, watoto wetu ndio wanakwenda, wakati huohuo Serikali inasisitiza chakula shuleni, sasa usalama utakuwaje?” amehoji.
Jumanne Shaaban, mkazi wa Mtaa wa Makanyagio wilayani humo, ameiomba Serikali kuboresha mazingira.
Vitus Mjelwa, mkazi wa Vwawa mkoani Songwe, amesema iwapo hali itakuwa mbaya ni vyema Serikali ikasitisha kwa muda kufungua shule kwa maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amethibitisha kuwapo kipindupindu katika halmashauri za Mbeya Jiji, Chunya na Mbeya Vijijini, akiwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari.
Amesema wakuu wa wilaya wameelekezwa kuketi haraka na kamati za afya kuhakikisha wanakabiliana na ugonjwa huo, ikiwamo shuleni na vyuoni.
“Hatua tulizochukua ni kufunga migahawa ambayo haina viwango, usitishaji vyakula maeneo ya mikusanyiko ikiwamo harusini, kuwatenga wagonjwa maeneo maalumu na kuzuia bidhaa kupangwa chini.
“Nimeelekeza wakuu wa wilaya zote na maofisa afya wakae kikao na wakuu wa shule zote binafsi na za Serikali ndani ya siku saba kujadili namna ya kukabiliana na hali hii kwa kuwa shule zinaenda kufunguliwa,” amesema.
Amesema iwapo kuna vifo basi havijaripotiwa na kwamba, Wizara ya Afya imefika Mbeya kuongeza nguvu.
Homera amesema visima vya kienyeji vimepigwa marufuku hadi kutolewe vibali ndipo vitumike.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amesema mazingira ya shule zote yameandaliwa vyema na tayari ametoa maelekezo kwa wakuu wa wilaya.
“Serikali tumejipanga vizuri kuhakikisha shule zitakapofunguliwa watoto wanahudhuria masomo yao bila changamoto yoyote kwani tayari nimetoa maelekezo kwa watendaji.
“Sehemu zote zenye mikusanyiko ya watu wahakikishe kunakuwepo na vifaa vya maji tiririka ili watu waweze kunawa mikono mara kwa mara,” amesema.
Amewataka wazazi na walezi kuruhusu watoto kwenda shule zitakapofungua akitoa onyo kwamba sheria itachukua mkondo wake kwa watakaowazuia.
Ofisa Elimu Jiji la Mbeya, Matilda Luvanda amesema wamejipanga kuhakikisha kila shule inakuwa na ndoo za maji kama ilivyokuwa wakati wa Uviko-19.
Amesema Alhamisi Januari 9, 2025 wanatarajia kuwa na kikao na wakuu wa shule, wasaidizi na wataalamu wa afya, akieleza pamoja na mambo mengine watajadili changamoto ya kipindupindu.
“Tunatarajia wanafunzi 11,914 kujiunga na kidato cha kwanza, miundombinu imeandaliwa vyema na Alhamisi tutakaa kikao kujadili taaluma na namna ya kukabiliana na kipindupindu” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbaraka Batenga amesema amefanya vikao na kamati za afya ngazi za kata na wilaya kuona njia bora ya kudhibiti na kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kutokomeza ugonjwa huo.
Amesema wametumia magari ya matangazo kutoa elimu kwa wananchi kufanya usafi wa mazingira, hususani kuwa na vyoo bora na kuvitumia na kunawa mikono kwa sababu na maji tiririka.
“Tunaendelea kutoa elimu kushirikiana na wataalamu wa afya japokuwa kuna tatizo maeneo ya porini vijana wanaofanya shughuli za utafutaji kukosa maeneo ya huduma ya choo,” amesema.
Imeandikwa na Saddam Sadick, Hawa Mathias na Idd Mumba