Hofu ya wanyama wakali yasababisha wazazi wa Same kujenga shule yao

Same. Wakazi wa Kitongoji cha Igoma, Kata ya Maore, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, wamelazimika kujenga shule yao ili kuwalinda watoto wao wanaotembea umbali mrefu kufuata shule dhidi ya hatari ya kushambuliwa na wanyama wakali.

Imeelezwa kuwa, wanafunzi wa Shule ya Msingi Njiro, iliyopo Kata ya Kisiwani, hulazimika kuamka usiku wa manane na kutembea kilomita 14 kila siku kwenda na kurudi shule, jambo linalohatarisha usalama wao kutokana na uwepo wa wanyama wakali kama tembo na faru.

Mbali na umbali mrefu, wanafunzi hao pia hukumbana na changamoto ya kuvuka korongo kubwa linalojulikana kama Nakombo wakati wa msimu wa mvua.

Korongo hilo hujaa maji, hali inayowafanya baadhi ya wanafunzi kushindwa kwenda shule kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Wakizungumza na Mwananchi Digital Januari leo Jumanne Januari 7, 2025, baadhi ya wananchi wamesema wamejichanga na kujenga vyumba vitatu vya madarasa ili kuwasaidia watoto hao kupata elimu bila kupitia changamoto kubwa za safari ndefu.

Julius Mtegwa, mwenyekiti mstaafu wa kitongoji hicho, amesema changamoto ya umbali wa shule iliwalazimu wananchi kuchanga fedha na kujenga shule itakayopunguza adha kwa watoto wao.

“Watoto wetu wamekuwa wakikabiliana na hatari ya kushambuliwa na tembo na nyati wanapokwenda au kurudi shuleni. Hali hii ilitufanya tuchukue hatua ya pamoja kujenga shule ili kuhakikisha watoto wanasoma katika mazingira salama,” amesema Mtegwa.

Silvano Mngara, mkazi mwingine wa kitongoji hicho, amesema mbali na hatari ya wanyama wakali, msimu wa mvua huongeza changamoto kubwa kwa sababu maji yanapoziba korongo, wanafunzi hushindwa kuvuka,hivyo kukosa masomo kwa muda mrefu.

Neema Msuya, mmoja wa wakazi hao amesema uwepo wa shule hiyo mpya utapunguza hofu kubwa waliyonayo wazazi wanapowaaga watoto wao alfajiri kuelekea shuleni.

Diwani wa kata hiyo, Rashid Gasper amewapongeza wananchi kwa jitihada zao za kuwekeza katika sekta ya elimu na kuahidi kushirikiana nao kuhakikisha shule hiyo inaanza rasmi kama shule shikizi kabla ya kujitegemea.

“Wananchi wamefanya kazi kubwa sana. Nitaendelea kuwasiliana na ofisa elimu wa wilaya ili kuhakikisha shule hii inatambuliwa rasmi na kuanza kutoa huduma mara moja,” amesema Diwani Gasper.

Ofisa Elimu wa Kata ya Maore, Steven Kihoko amethibitisha kuwa, mchakato wa kuifanya shule hiyo kuwa shule shikizi unaendelea na taarifa zimeshawasilishwa kwa mamlaka husika kwa hatua zaidi.

Related Posts