Baada ya kuanza kibarua chake, Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Aman Josiah, amesema licha ya ugeni alionao kwenye Ligi Kuu Bara, lakini haoni kitu kipya badala yake anaamini katika uwezo wake.
Josiah ameanza kazi hiyo kikosini humo akitokea Geita Gold inayoshiriki Ligi ya Championship, akichukua nafasi ya Mbwana Makata aliyesitishiwa mkataba Desemba 28, 2024 kufuatia matokeo yasiyoridhisha.
Akizungumza leo Januari 7, 2025, baada ya mazoezi ya timu hiyo, Josiah amesema pamoja na kuwa mara ya kwanza kuongoza timu ya Ligi Kuu, lakini uwezo wake na imani aliyopewa haoni kitu kipya bali ni kujiamini.
Amesema anafahamu ugumu alionao kutokana na matokeo ya timu yalivyo huku akieleza ushirikiano alioupata haswa kwa wachezaji waandamizi waliorejea kutoka majeruhi.
“Ni namna nitakavyowatumia wachezaji, bahati nzuri nimeona hata waliokuwa majeruhi wamerejea, sioni kitu kipya kwakuwa nimeaminiwa lazima nifanye kazi.
“Kwakuwa tupo katika kipindi cha usajili, tayari nimeongea na viongozi kujua wapi tuboreshe kikosi, kwa ujumla matarajio ni kufanya vizuri,” amesema Josiah.
Kocha huyo aliyewahi kuzinoa Biashara United, Pamba (kwa sasa Pamba Jiji), Tunduru Korosho na Geita Gold, ameongeza kuwa licha ya muda kutotosha lakini hadi kufikia Machi 1 mwaka huu ligi itakapoendelea atakuwa amepata pakuanzia.
Nahodha wa timu hiyo, Salum Kimenya amesema kwa sasa wanampa ushirikiano kocha huyo akieleza kuwa wanaendelea kuipambania Prisons kuhakikisha mzunguko wa pili wanasahihisha makosa.
“Tunamkaribisha kocha mpya, tunashukuru baadhi ya tuliokuwa majeruhi tumerejea, tunaamini tutafanya vizuri,” amesema beki huyo mkongwe kikosini humo.
Naye kipa wa timu hiyo, Edward Mwakyusa amesema hawakuwa na mwanzo mzuri, lakini kwa muda huu ligi imesimama watajifua vyema kuhakikisha wanarejesha heshima.
“Mashabiki wawe na matarajio makubwa, tutatumia vyema muda huu kujifua ili kupata matokeo mazuri mzunguko wa pili, hatujakata tamaa na morali ipo juu,” amesema kipa huyo.
Tanzania Prisons ipo nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara kati ya timu 16 ikiwa na pointi 14 baada ya kucheza mechi 16, imeshinda tatu, sare tano na kupoteza nane. Bado mechi 14 za kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja kwani ilipo sasa ni katika mstari wa kucheza mechi za mtoano kuepuka kushuka.