BAADA ya jana Jumatatu michuano ya Kombe la Mapinduzi 2025 kuendelea kwa mzunguko mwingine baada ya Januari 3 na 4 kupigwa mechi mbili, leo ni zamu ya Kilimanjaro Stars dhidi ya Kenya kujiuliza.
Mchezo huo unatarajiwa kuanza kuchezwa saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Gombani uliopo Kisiwani Pemba ukizikutanisha timu ambazo kila moja inahitaji ushindi kujitengenezea nafasi ya kucheza fainali.
Kilimanjaro Stars ambayo inaundwa na wachezaji kutoka Tanzania Bara, ilipoteza mchezo wa kwanza kwa bao 1-0 dhidi ya Zanzibar Heroes huku Kenya ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Burkina Faso.
Kipigo cha Kilimanjaro Stars kimewafanya kubaki njiapanda kuelekea mchezo wa leo kwani ikipoteza tena haitakuwa na nafasi ya kucheza fainali ikiiacha Kenya kuwa na matumaini hayo.
Katika msimamo wa michuano hiyo inayoshirikisha timu nne, kabla ya mechi moja ya jana haijachezwa kati ya Zanzibar Heroes na Burkina Faso, vinara walikuwa Zanzibar Heroes wenye pointi tatu, wakifuatiwa na Burkina Faso na Kenya wote wakiwa na pointi moja wakati Kilimanjaro Stars haina kitu.
Kuelekea mchezo huo wa leo, Kocha wa Kilimanjaro Stars, Ahmad Ally, alisema wanatarajia ushindani mkubwa kutokana na uimara wa wapinzani wao.
“Hautakuwa mchezo rahisi kutokana na wapinzani wetu tulivyowaona walivyocheza mechi yao, hivyo tunahitaji kujitoa kwa asilimia mia mchezo wa kesho (leo) tupate ushindi.
“Kama nilivyosema, Kenya wapo vizuri vipindi vyote, wanapokuwa na mpira na wanapokuwa hawana, tumeangalia kila kitu kuhusu wao ili kuona jinsi gani tutakuwa bora dhidi yao na kufanya vizuri.”
Kwa upande wa Kocha wa Kenya, Fransi Kimanzi, alisema: “Tumeendelea kujiandaa kufanya vizuri, tunaamini mchezo wa kesho (leo) utakuwa mzuri na kuwaburudisha mashabiki.”
Baada ya mechi moja ya leo, kesho Jumatano ni mapumziko kisha michuano hiyo itaendelea Januari 9 kwa Kilimanjaro Stars kukabiliana na Burkina Faso, huku Januari 10 ikiwa zamu ya Zanzibar Heroes dhidi ya Kenya. Timu mbili zitakazokuwa na pointi nyingi baada ya hapo, zitacheza fainali Januari 13.