Kocha Singida Black Stars ataka ushindi, burudani

MMESIKIA huko? Kocha mpya wa Singida Black Stars, Hamdi Miloud mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa, ambaye amerithi mikoba ya Patrick Aussems, ameeleza kuwa na mpango wa kuifanya timu hiyo kuwa tishio Ligi Kuu Bara kulingana na ubora wa wachezaji alionao.

Kocha huyo mwenye leseni ya UEFA A, anasisitiza kuwa lengo lake ni kuleta mabadiliko makubwa kwa Singida Black Stars kwa kutambulisha mfumo wa soka la kuvutia, lenye mashambulizi ya nguvu na ulinzi imara.

Akizungumza na wachezaji wake baada ya kuanza kambi ya maandalizi kujiandaa na ligi itakayoendelea Machi Mosi mwaka huu, Miloud alisema: “Tuna timu yenye vipaji vikubwa na nimejionea uwezo wao. Mchezo wa soka si kushinda tu bali ni kuhusu kutoa burudani kwa mashabiki. Lengo langu ni kuhakikisha timu yangu inacheza soka la kuvutia ambalo litawafanya mashabiki wa Singida Black Stars kujivunia timu yao.”

Kocha Miloud aliongeza kuwa ili kufikia malengo haya ya juu, itahitajika kazi ya ziada, umoja na kujituma kutoka kwa kila mchezaji.

“Hatutakuwa na njia ya mkato katika kufanikisha malengo yetu. Kila mchezaji atahitajika kuonyesha kiwango cha juu cha ufanisi. Timu yangu itacheza soka la kushambulia, lakini pia tutakuwa na umakini mkubwa katika ulizi,” alisema Miloud.

Miloud pia amewataka wachezaji wake kuwa tayari kwa mabadiliko makubwa katika jinsi wanavyocheza, akisisitiza kuwa soka safi na la kuvutia litakuwa msingi wa timu hiyo.

“Nina imani kubwa na wachezaji wangu. Kila mmoja wao ana kipaji cha kipekee, tunahitaji kuwa na ushirikiano mzuri uwanjani ili tufikie malengo yetu,” alisema kocha huyo.

Katika kuhakikisha kuwa malengo ya timu yanatimia, Singida Black Stars imemsajili mshambuliaji Jonathan Sowah kutoka Al-Nasr ya Libya. Mshambuliaji huyu anatarajiwa kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, ambayo tayari inasifika kwa kuwa na nyota kama Elvis Rupia, anayeshika nafasi ya kwanza katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu Bara akifunga mabao manane.

Related Posts