Pyongyang. Korea Kaskazini imerusha kombora la masafa ya kati ikiwa ni mwendelezo wa majaribio yake ya silaha.
Kombora hilo limerushwa wakati ambao Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken anaendelea na ziara yake nchini Korea Kusini.
Taarifa iliyotolewa jana Jumatatu Januari 6, 2025 na Jeshi la Korea Kusini ilisema kombora hilo lilielekezwa upande wa Mashariki ya Korea Kaskazini muda mfupi baada Blinken kuanza mazungumzo na Rais wa Mpito wa Korea Kusini, Choi Sang-mok.
“Jeshi letu lilinasa taarifa ya kurushwa kwa kombora la masafa ya kati kutoka nchini Korea Kaskazini,” ilisema taarifa ya Jeshi hilo na kuripotiwa na tovuti ya Al Jazeera.
Taarifa ya Jeshi la Korea Kusini pia imesema kombora hilo la majaribio, linaelezwa kwenda umbali wa Kilometa 1,100 (maili 680), kabla ya kutua ardhini na kupiga baharini eneo la Peninsula ya Korea na Japan huku ikidokeza kuwa ufuatiliaji wa kina unaendelea.
Hata hivyo, vyanzo vya habari nchini Japan vinasema kombora hilo lilipiga baharini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa Umma na Wizara ya Ulinzi ya Japan, Kombora hilo la Korea Kaskazini lilipiga eneo la kibiashara katika bahari na kudai hakuna madhara yoyote yaliyoripotiwa kwenye vyombo vya majini.
Tayari Blinken na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini, Cho Tae-yul walipozungumza na vyombo vya habari wamelaani jaribio hilo, huku wakisema kitendo cha Korea Kaskazini kufanya hivyo imekiuka maekezo ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Urushaji wa kombora hilo jana Jumatatu ni wa kwanza mwaka huu 2025, tangu Korea Kaskazini ilipofanya hivyo Novemba 5, 2024 ambapo ilifanya majaribio ya kombora la masafa mafupi kuelekea katika visiwa vilivyoko mashariki mwa taifa hilo.
Mwandishi wa Al Jazeera, Patrick Fok, akiripoti kutokea Seoul amesema kurushwa kwa kombora hilo kulifanyika makusudi na kwa malengo mahsusi.
“Ukiangalia jaribio la kombora hilo limefanyika zikiwa zimebaki siku chache hadi kuapishwa kwa Donald Trump kuwa Rais wa Marekani.
“Jaribio hilo pia ni la muhimu kwa Korea Kaskazini kwa sababu ilikuwa imepoa sana tangu kuibuka kwa mtikisiko wa kisiasa nchini Korea Kusini,” aliripoti mwandishi huyo.
Bunge la Korea Kusini lilipiga kura ya kumng’oa madarakani Rais Yoon Suk Yeol na kumzuia kutekeleza majukumu yake tangu Desemba 3, 2024 muda mfupi baada ya uamuzi wake wa kuiweka nchi hiyo chini ya Sheria ya Kijeshi (Martial Law).
Hadi sasa kesi ya kung’olewa madarakani kwa Yoon inaendelea kusikilizwa katika Mahakama Maalum ya Katiba nchini humo, huku maofisa wa Kitengo cha Kupambana na Rushwa nchini humo wakiendelea na jitihada za kumkamata Rais huyo.
Kwenye mazungumzo yao, Blinken amemuahidi Rais wa Mpito, Choi Sang-mok kuwa Marekani itaendelea kushirikiana na taifa hilo hususan ni kwenye sekta ya ulinzi na usalama na kuendeleza ushirikiano na Japan.
Katika hatua nyingine, Blinken amesema anaamini Russia itaendelea kushirikiana na Korea Kaskazini hususan ni kuendelea kubadilishana wanajeshi kwa ajili ya mapigano yanayoendelea kati ya taifa hilo la Ukraine.
“Jeshi la Korea Kaskazini tayari limeanza kupokea vifaa vya kijeshi na mafunzo kutoka Russia. Sasa tuna kila sababu ya kuamini kwamba Moscow inalenga kushirikiana kwenye masuala ya anga na Pyongyang,” amesema Blinken.
Blinken alitumia jukwaa hilo kusema kuwa zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Korea Kaskazini waliopelekwa Russia wameuawa ama kujeruhiwa katika mashambulizi ya Ukraine eneo la Mkoa wa Kursk.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.