Maagizo ya Rais Samia, Dk Mwinyi uwekezaji visiwani

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amefungua hoteli akiunga mkono kauli ya Rais Dk Hussein Mwinyi wa Zanzibar, kwamba wanaochelewesha uwekezaji katika visiwa baada ya miezi mitatu wavirudishe serikalini watafutwe wawekezaji wengine.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Januari 7, 2025 alipokuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mradi wa Hoteli ya Bawe Island by Cocoon Collection.

Muonekano wa Hoteli ya Kitalii ya Bawe Island the Cocoon Collection iliyopo katika Kisiwa cha Bawe, Zanzibar 

Mradi huo umejengwa katika Kisiwa cha Bawe kilichopo Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.

“Naungana na Rais wa Zanzibar wale wote waliopewa visiwa na hawajafanya kazi basi miezi mitatu ikifika Rais Mwinyi usirudi nyuma. Wawekezaji wako wengi hawa, kama hawajawekeza acha tutafute wawekezaji wa kweli,” amesema Rais Samia.

Awali, Dk Mwinyi aliwataka wawekezaji waliokodishwa visiwa na hawajaanza ujenzi baada ya miezi mitatu Serikali ivichukue.

“Muda umeshakuwa mrefu na hawajaanza kujenga, Serikali inawapa miezi mitatu kuanzia sasa baada ya hapo kama hawajaanza ujenzi visiwa hivyo vitarudishwa serikalini ili wapewe watu wenye uwezo. Kwa wale ambao tayari tunawashukuru na kuwapongeza,” amesema Dk Mwinyi.

Muonekano wa Hoteli ya Kitalii ya Bawe Island the Cocoon Collection iliyopo katika Kisiwa cha Bawe, Zanzibar 

Hata hivyo, Rais Samia amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi 15 ya uwekezaji iliyopo kwenye visiwa vidogo vidogo vya Zanzibar.

Amesema mradi huo umetoa ajira 400 kwa Watanzania na kuinua mapato kutokana na kodi na kutangaza visiwa vya Zanzibar.

Rais Samia  amesema wawekezaji wa mradi wa Bawe wameshawekeza Dola 42 milioni za Marekani (Sh104 bilioni).

“Wana miradi ya kutengeneza umeme wa jua, mradi wa kutoa chumvi kwenye maji na kuyatumia kwenye hoteli,” amesema Rais Samia.

Amesema sera na imani kwa Serikali ndiyo inafanya wawekezaji waendelee kuamini kuwekeza nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, Mwekezaji wa Hoteli ya Kitalii ya Bawe Island the Cocoon Collection, Andrea Azzola wakati wa ufunguzi wa Hoteli Bawe Island the Cocoon Collection iliyopo katika Kisiwa cha Bawe, Zanzibar

Kwa upande wake, Dk Mwinyi amesema fursa zilizopo katika mradi zinakwenda kwa wananchi moja kwa moja kuanzia kwa wanaofanya shughuli za uvuvi.

“Wananachi waliokuwa wanafanya shughuli za uvuvi hapa wamejengewa sehemu nzuri kwa ajili ya shughuli zao, samaki wote wanaowapata wanakuja kuuza,” amesema.

Amesema faida za uwekezaji ni ajira kutolewa kwa wananchi, akitoa rai watu wasome ili wapate ajira zaidi katika hoteli zinazojengwa Zanzibar.

“Faida nyingine ni kukua kwa soko la bidhaa na kuongezeka kwa watalii. Utalii ndiyo sekta mama ya nchi, hivyo wakiongezeka na uchumi unaongezeka,” amesema.

Related Posts