Madaktari wa wanyama 120 waondolewa sifa

Dar es Salaam. Baraza la Veterinari Tanzania (TVA) limewafutia usajili madaktari wa wanyama 120 kwa kushindwa kutimizwa matakwa ya sheria ya baraza hilo.

Uamuzi wa kuwaondolea sifa wataalamu hao umefikiwa na baraza hilo katika kikao chake kilichoketi Desemba 23, 2024.

Taarifa iliyotolewa Desemba 30, 2024 na Baraza la Vetenari, inaeleza kuwa, kwa mamlaka iliyopatiwa kwa kifungu 25 (a), (b)(i)(ii) ya Sheria ya Veterinaria, sura 319, taarifa inatolewa kwa umma ya kuwa usajili wa madaktari wa wanyama 120 umefutwa.

“Baraza la Veterinari Tanzania katika kikao kilichofanyika Desemba 23, 2024 majina ya madaktari hao yameondolewa kwenye rejesta ya madaktari,” inaeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kutoka ofisi ya Msajili wa Baraza la Vetenari madaktari hao hawaruhusiwi kujihusisha na shughuli yoyote inayohusiana na utoaji wa huduma ya afya ya wanyama.

“Majina ya madktari wa wanyama waliofutwa kwenye rejesta yameambatishwa na pia yanapatikana kwenye ya Baraza la Veterinari ambayo ni www.vct.go.tz,” imeandikwa kwenye taarifa hiyo.

Baraza la Vetenari Tanzania limeundwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Veterinari, sura 319 likiwa na jukumu la kusimamia wataalamu wa afya ya wanyama na utolewaji wa huduma ya afya ya wanyama nchini.

Related Posts