Moshi. Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kilimanjaro, limeendelea na operesheni maalumu ya kuhakiki leseni za madereva wa magari ya abiria.
Jeshi hilo limesema madereva watakaokutwa hawana sifa za kuendesha magari hayo wataondolewa barabarani.
Jana, Januari 6, 2025 baadhi ya magari madogo aina ya Toyota Noah yanayobeba abiria kati ya Moshi Mjini na Rombo, yalifanyiwa ukaguzi maalumu.
Hatua hiyo ilisababisha kusimama kwa muda kwa shughuli za usafirishaji, hali iliyosababisha usumbufu kwa abiria katika stendi ndogo ya magari mjini Moshi.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Januari 7, 2025, Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani mkoani hapa, Nassoro Sisiwaya amesema kwa madereva ambao wana leseni na hawana vyeti vya udereva au hawakusomea udereva wataondolewa barabarani.
“Tumeendelea kuhakiki magari ya abiria katika mkoa wetu wa Kilimanjaro na kila tunayemhakiki kama ana changamoto tunamwondolea daraja, kwa mfano kama una cheti na una madaraja ambayo hayastahili tunaondoa, kama ulikuwa unaendesha Noah utaendesha gari dogo,” amesema Kamanda Sisiwaya.
Amesema lengo la ukaguzi huo ni kuondoa madereva wote ambao hawana sifa barabarani kwa kuwa, ndio wanaoonekana kusababisha ajali nyingi za barabarani.
Hata hivyo, amesema katika ukaguzi ambao wameshaufanya, baadhi ya madereva wana sifa lakini tatizo lililobainika huwa hawajitokezi kuhakiki leseni zao.
Dereva Joseph Tarimo amesema kuna wenzao hawana sifa za kuendesha magari ya abiria na hao ndiyo chanzo cha matatizo yanayotokea barabarani.
“Madereva ambao hawana sifa wapo na hata tukikaguliwa hatukosekani, wengine wanaendesha tu kwa sababu ya uzoefu wao, lakini hawana taaluma ya barabarani,” amesema Tarimo.
Naye, Nelson Mwarami dereva wa basi anayefanya safari zake kati ya Moshi Mjini na Arusha, amesema kila dereva mwenye taaluma yake, anapaswa kuzingatia ukaguzi wa chombo chake na leseni yake kwa usalama wa abiria.
Wakati huohuo, baadhi ya wasafiri wanaosafiri kutoka Sanya juu kwenda Ngarenairobi, Wilaya ya Siha, wamelalamikia kupanda kwa nauli kutoka Sh1,000 hadi Sh3,000 na wameiomba mamlaka husika kuingilia kati.
Mmoja wa wasafiri hao, Samweli Mbise mkazi wa Ngarenairobi amesema wanatozwa nauli kati ya Sh2,000 hadi Sh3,000 badala ya Sh1,000 kutoka Sanya juu hadi Ngarenairobi jambo ambalo sio sahihi.
“Wakati mwingine ukimhoji kondakta wa gari anakutishia kukushusha au anakwambia usipande gari yake kama huna hiyo fedha, wakati mwingine kwa sababu ya umbali na ni usiku, unalazimika kutoa hivyo hivyo ili ufike nyumbani,” amesema msafiri huyo.
Akizungumzia hilo, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra) Mkoa wa Kilimanjaro, Paulo Nyello amewataka wananchi pindi wanapopanda magari wahakikishe wanaangalia nauli elekezi ubavuni mwa gari.
Amesema wakitozwa zaidi ya nauli elekezi wanapaswa kutoa taarifa kwa mamlaka hiyo.
“Abiria kabla ya kupanda gari jiridhishe kwanza, angalia ubavuni nauli zimeandikwa kila kituo na pia namba za Latra zipo kupiga ni bure, tutadhibiti hali hiyo na tutachukua hatua kwa gari husika,” amesema Nyello.