Dodoma. Mrithi wa Abdulrahman Kinana ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika nafasi ya Makamu Mwenyeiti-Bara atajulikana kati ya Januari 18-19, 2025 kwenye mkutano mkuu maalumu utakaofanyika jijini Dodoma.
Nafasi hiyo ya Makamu Mwenyekiti imekuwa wazi tangu Julai 28, 2024 baada ya Kinana kuandika barua ya kuomba kujiuzulu wadhifa huo kwenda kwa Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.
Kinana aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, alirejea kwenye nafasi ya Makamu mwenyekiti Aprili 1, 2022 alipochaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu kwa kura za ndio 1,875 sawa na asilimia 100.
Alichaguliwa akichukua nafasi ya Philip Mangula ambaye aliandika barua ya kung’atuka kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia ambaye aliridhia.
Tangu Kinana alipojiuzulu, nafasi hiyo imebaki wazi kwa kipindi cha takriban miezi mitano, jambo ambalo ni la kipekee katika historia ya chama hicho.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, nafasi ya makamu mwenyekiti ni muhimu katika kumsaidia mwenyekiti wa chama kutekeleza majukumu yake.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Makamu wa Mwenyekiti watakuwa ndio wasaidizi wakuu wa mwenyekiti na watafanya kazi zote za CCM watakazopewa na mwenyekiti.
Haikuwa mara ya kwanza kujiuzulu kwani Mei 28, 2018, aliandika barua ya kujiuzulu nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM kwa Rais wa wakati huo, John Magufuli. Mei 29, 2018, nafasi yake ilichukuliwa na Dk Bashiru Ally.
Leo Jumanne, Januari 7, 2025, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amekutana na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho jijini Dodoma na kutangaza kufanyika kwa mkutano mkuu maalumu.
Makalla amesema mojawapo ya ajenda ya mkutano huo utakaofanyika Januari 18-19, jijini Dodoma ni kumpata makamu mwenyekiti wa chama hicho baada ya Kinana kuomba kupumzika.
Amesema kumekuwa na taarifa nyingi kuhusu nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama hicho, huku wengine wakifika mbali zaidi na kutoa utabiri wa mtu atakayemrithi Kinana bila kufahamu utaratibu wa kumpata atakayeshika nafasi hiyo.
“Nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM haigombewi wala hakuna mtu anayejaza fomu kuwania nafasi hiyo, kazi ya kumpata atakayerithi nafasi hiyo inafanywa na vikao vya kamati kuu na Halmashauri kuu ya Taifa ambapo wataleta jina lake kwenye mkutano mkuu na atapigiwa kura huko,” amesema Makalla.
Amesema hayo mengine yanayoendelea ya utabiri wa atakayerithi nafasi hiyo hayana maana kwani mpaka sasa bado hajajulikana.
Makalla amesema vikao vya kamati kuu na Halmashauri kuu vitakutana Januari 16, 2025.
Aidha amesema ajenda nyingine ambazo zitajadiliwa kwenye mkutano huo ni pamoja na kupokea kazi zilizofanywa na CCM kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2022 hadi 2025 na kupokea utekelezaji wa ilani ya chama hicho kwa upande wa Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Kwa hiyo nawakaribisha wajumbe wote wa mkutano mkuu pamoja na wajumbe waalikwa kwenye mkutano huu ambao maandalizi yake yameshakamilika chini ya Katibu Mkuu Dk Emmanuel Nchimbi,” amesema Makalla.
Licha ya Makalla kueleza hayo, lakini kumekuwa na baadhi ya majina makubwa ndani ya CCM yanatajwa kurithi nafasi hiyo ya juu ndani ya chama hicho hususan kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Miongoni mwa majina hayo ni mawaziri wakuu wastaafu, Mizengo Pinda na Fredrick Sumaye ambao kila mmoja anahistoria ndefu ya uongozi ndani ya Serikali na chama.
Wengine ni mwenyekiti wa zamani wa Jumuiya ya Wazazi wa chama hicho, Abdallah Bulembo ni kada mwenye uzoefu wa muda mrefu katika siasa za chama huku Rajabu Abdrahman ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu akitajwa kuvaa viatu vya Kinana.
Wengine wanaotajwa ni Steven Wassira ambaye ni mwanasiasa mkongwe aliyeshika nafasi nyingi za uongozi ndani ya Serikali na chama tangu enzi za uongozi wa Mwalimu Nyerere. Paul Kimiti, kada mwenye historia ndefu ya uongozi ndani ya CCM na Serikali, pamoja na kuwa msaidizi wa Mwalimu Nyerere katika masuala ya chama.
Profesa Mark Mwandosya, kada mwenye historia ya kushika nafasi mbalimbali serikalini, ikiwa ni pamoja na uwaziri, na pia ndani ya CCM.