Wakati Rais mteule wa Marekani, Donald Trump akisubiri kuapishwa Januari 20, mwaka huu, bado anakabiliwa na uwezekano wa kuhukumiwa wiki hii kwenye kesi yake ya kumlipa kahaba, baada ya jaji kukataa kusitisha hukumu yake licha ya mawakili wake kukata rufaa.
Katika kesi hiyo, Trump anatuhumiwa kumlipa Stormy Daniels ili kumziba mdomo kuhusu kuwapo kwa uhusiano kati yao.
Jaji wa Mahakama ya Manhattan, Juan Merchan, ameamuru usomwaji wa hukumu hiyo uendelee kama ulivyopangwa Ijumaa Januari 10, ikiwa ni wiki moja tu kabla ya kuapishwa kwa Trump kuwa rais.
Jaji huyo amekataa shinikizo la mawakili wa Trump ambao wamekata rufaa kuitaka Mahakama ya Rufaa kuifuta hukumu ya awali, iliyomtia hatiani mteja wao.
Ikiwa hukumu hiyo itasomwa, Trump atakuwa rais wa kwanza kuchukua madaraka akiwa ametiwa hatiani kwa uhalifu.
Hata hivyo, Jaji Merchan ameandika kwamba hakuwa na nia ya kumhukumu Trump kifungo gerezani na kwamba hukumu ya “kuachiliwa bila masharti” ikimaanisha hakuna kifungo, faini ya fedha ingekuwa suluhisho linalowezekana zaidi.”
Kutolewa kwa hukumu hiyo kutafungua njia kwa Trump kukata rufaa.
Merchan alikiri katika uamuzi wake kwamba Trump ameweka wazi nia yake ya kukata rufaa.
Kesi inayomsubiri kwa sasa Trump ni ya malipo ya pesa kwa nyota wa filamu za utupu ili kumziba mdomo, ambayo Mahakama ya New York imemkuta na hatia.
Kwa mujibu wa BBC, ikiwa Trump atahukumiwa kifungo gerezani, mawakili wake wataka rufaa dhidi ya hukumu hiyo mara moja kwa hoja kuwa kifungo hicho kitamzuia kutekeleza majukumu yake rasmi.
“Mchakato wa kukata rufaa katika kesi hiyo unaweza kuendelea kwa miaka,” anasema mwendesha mashtaka wa zamani wa Brooklyn, Julie Rendelman, alipozungumza na BBC.
Mbali na kesi hiyo, Trump pia ametiwa hatiani katika makosa 34 ya kughushi rekodi za biashara yake Mei 2024 jijini New York.
Kesi ya kumpindua Rais Biden
Pia, anakabiliwa na tuhuma za kutaka kupindua ushindi wa Rais Joe Biden katika uchaguzi wa mwaka 2020, kesi iliyofunguliwa na wakili maalumu, Jack Smith.
Hata hivyo, kesi hiyo imekuwa na mtafaruku wa kisheria tangu Mahakama ya Juu ilipotoa uamuzi, msimu huu wa joto kwamba Trump kwa namna fulani ana kinga ya kutofunguliwa mashitaka ya jinai kwa vitendo alivyofanya akiwa madarakani.
Smith amewasilisha tena kesi yake, akisema jaribio la Trump la kubatilisha uchaguzi halikuhusiana na majukumu yake rasmi.
Hata hivyo, mwendesha mashtaka wa zamani nchini humo, Neama Rahmani amesema, Trump akiwa rais mteule, kesi ya jinai kwake inaweza kuondoshwa.
“Iko wazi kuwa rais aliye madarakani hawezi kushtakiwa, hivyo kesi juu ya uchaguzi katika Mahakama ya Wilaya ya DC itaondoshwa,” amesema.
Rahmani amesema iwapo Smith atakataa kutupilia mbali kesi hiyo, Trump anaweza kumuondoa, kama alivyoahidi kufanya.
“Nitamfuta kazi ndani ya sekunde mbili,” Trump alisema wakati wa mahojiano ya redio Oktoba 2024.
Smith pia, anaongoza kesi dhidi ya Trump juu ya tuhuma za kuzishughulikia vibaya hati za siri baada ya kuondoka Ikulu ya White House, mashtaka hayo Trump anayakanusha pia.
Inaelezwa alizihifadhi hati nyeti nyumbani kwake Mar-a-Lago na kutatiza juhudi za Idara ya Haki kuzipata hati hizo.
Jaji aliyepewa kesi hiyo, aliyeteuliwa na Trump, Aileen Cannon, alitupilia mbali mashtaka Julai, akisema Smith aliteuliwa isivyofaa na Idara ya Haki kuongoza kesi hiyo.
Smith alikata rufaa dhidi ya uamuzi huo, lakini kwa vile Trump anarudi kuchukua madaraka, mazungumzo sasa yanaendelea kuhusu kuimaliza kesi hiyo.
Rahmani amesema, anatarajia kesi ya hati za siri itafikia hatima sawa na kesi ya uchaguzi.
Trump pia, anakabiliwa na mashtaka ya jinai katika Jimbo la Georgia kuhusu juhudi zake za kupindua matokeo ya uchaguzi wa 2020 katika jimbo hilo.
Kesi hiyo imekumbwa na vikwazo vingi, ikiwa ni pamoja na jitihada za kumwondolea sifa Mwanasheria wa Wilaya, Fani Willis juu ya uhusiano wake na wakili aliyemwajiri kufanyia kazi kesi hiyo.
Mahakama ya rufaa iko mbioni kutathmini iwapo Willis aruhusiwe kuendelea na kesi hiyo au la.
Lakini kwa vile Trump ndiye rais ajaye, kesi hiyo inaweza kukabiliwa na ucheleweshaji zaid , au ikiwezekana kufutwa.
Inatarajiwa kusitishwa wakati Trump akiwa madarakani, kulingana na wataalamu wa sheria.
Rais mteule Donald Trump atahukumiwa Januari 10 katika kesi ya jinai kwa kupatikana na hatia kwa mashtaka yanayohusiana na pesa za kuficha ukweli zilizolipwa kwa nyota wa filamu za watu wazima.