Nabi atuma ujumbe mzito Yanga, amtaja Ramovic

MASHABIKI wa Yanga wameanza kuchekelea wakisahau siku ngumu walizopitia kabla na baada ya kuondoka kwa kocha wao Miguel Gamondi kisha nafasi yake kuchukuliwa na Sead Ramovic ambaye naye alikuwa kama hawamuelewi vile akianza vibaya.

Sasa baada ya mambo kukaa sawa, aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Nasredine Nabi ambaye bado anapigana vita ngumu akiwa na timu yake ya Kaizer Chiefs, alisema alikuwa anajua kwamba Ramovic atatuliza upepo wa timu hiyo licha ya kuanza vibaya.

Nabi alisema alikuwa ana imani hiyo kutokana na kujua soka la Tanzania ambapo pia alikuwa anazifahamu falsafa za kocha huyo ambaye amewahi kufanya kazi nchini Afrika Kusini kabla ya kutimkia Tanzania.

Mtunisia huyo alisema baada ya Yanga kuanza kucheza soka la maana na Ramovic kujipata, Yanga itaendelea kufanya vizuri kwa kuwa falsafa za kocha huyo Mjerumani zitazipa shida timu nyingi.

“Nilikuwa sina wasiwasi, nilisema hata mimi sikuanza vizuri nilipokuwa Yanga, kila kitu kinakwenda kwa hatua, unaona hata mimi hapa Kaizer Chiefs sijaanza vizuri kama ninavyotaka lakini naijua sababu na ni suala la muda kwa kuwa tunahitaji kubadilisha sana hii timu,” alisema Nabi na kuongeza.

“Ramovic aina ya soka analotaka timu yake icheze nilikuwa nafahamu kwamba itawarudisha Yanga kwenye mstari, nawapenda mashabiki wa Yanga siwezi kuwaambia uongo, walitakiwa kuwa wavumilivu nadhani sasa wanafurahi. Sikuona tatizo juu ya uzoefu wake nilijua kama wachezaji wakimsikiliza na kushika anachotaka Yanga itaendelea kuwa tishio, naijua Ligi ya Tanzania, kwa soka la Ramovic atasumbua sana.”

Ramovic amepoteza mechi mbili zote za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ambayo iliwapa wasiwasi mashabiki wa timu hiyo lakini baadaye akashinda mechi sita zilizofuatia katika michuano tofauti huku akitoa sare moja ndani ya mechi tisa. Nabi aliongeza kuwa anaheshimu kazi iliyofanywa na kocha aliyepita Gamondi lakini ameona Yanga imeanza kurudi kwenye ubora wake kwa wachezaji kucheza kikubwa.

Yanga kwa sasa ina kibarua cha kwenda Mauritania kucheza dhidi ya Al Hilal mechi ya tano ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika Kundi A kupambania nafasi ya kufuzu robo fainali.

Kuelekea mchezo huo sambamba na ule wa mwisho nyumbani dhidi ya MC Alger utakaochezwa Januari 18, Ramovic anaifukuzia rekodi ya Gamondi ambaye msimu uliopita aliifikisha Yanga robo fainali ya michuano hiyo akiwa kocha wa kwanza kikosini hapo kufanya hivyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Related Posts