PLANET imetwaa ubingwa wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Mwanza (MRBA), baada ya kuifunga Eagles katika michezo 3-1.
Fainali ya mchezo huo iliyochezwa kwa timu kucheza michezo mitano yaani best of five play off ilimalizika katika Uwanja wa Mirongo jijini humo.
Katika mchezo wa kwanza Planet ilishinda kwa pointi 71-53, ule wa pili 67-62, huku Eagles iliyokuwa bingwa mtetezi wa ligi hiyo ikishinda katika fainali ya tatu kwa pointi 63-55, ilhali ile ya nne Planet ikashinda kwa pointi 64-54.
Mchezaji bora wa mashindano hayo (MVP), alichaguliwa kuwa Joseph Carlos wa Planet, huku chipukizi akiwa Kassimu Mansour wa Young Profile.
Akizungumza na Mwanasposti, katibu msaidizi wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Benson Nyasebwa, alisema timu zote zilionyesha viwango vikubwa ikiashiria kwamba siku za usoni nchi itakuwa na mastaa wengi bora wa mchezo huo.
“Nimeona ushindani ulikuwa mkubwa sana na imeonyesha ni jinsi gani mchezo wa kikapu unavyokua mkoani humo,” alisema Nyasebwa.