Kenya. Wakati vijana wanne waliokuwa wamedaiwa kutekwa nyara wakiachiliwa katika maeneo tofauti nchini Kenya, polisi wamekana kuwateka au kuwaachia huru.
Vijana hao wanne kati ya 29 walioripotiwa kutekwa na watu wasiojulikana wamepatikana wakiwa hai jana Januari 6, 2025, tovuti za Daily Nation na Tuko zimeripoti.
Vijana hao wanaotajwa kuwa wakosoaji wa Serikali ya awamu ya tano ya nchi hiyo, walianza kutoweka mwishoni mwa mwaka 2024, jambo lililosababisha baadhi ya Wakenya kuandaa maandamano kuitaka Serikali iwarudishe.
Vijana hao ni Billy Munyiri Mwangi (24), Peter Muteti (22), Bernard Kavuli na Ronny Kiplagat.
Katika sakata hilo, leo Januari 7, 2025 kupitia Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), polisi wamekanusha vikali kuhusika au kuwaachilia vijana hao.
Kwa mujibu wa Gazeti la Taifa Leo, Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) imejitenga na utekaji nyara unaoripotiwa.
Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, amesema hakuna kituo chochote cha polisi kilichokuwa kikiwazuia vijana hao na Rais William Ruto akasisitiza kuwa Serikali yake haihusiki na vitendo vilivyo nje ya katiba na sheria.
Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu (KNHRC), imesema kuna matukio 82 vya utekaji nyara yameripotiwa tangu Juni 2024.
Kwa jumla, watu 25 waliotoweka tangu Juni mwaka jana wakati wa maandamano ya Gen Z, bado hawajulikani walipo.
Aidha, NPS imehakikisha kwamba maofisa wake watawasiliana na watu walioripotiwa kutoweka katika vituo mbalimbali vya polisi, vikiwamo Embu, Kabete na Thogoto. Lengo ni kusaidia uchunguzi unaoendelea kuhusu kupotea kwao.
Hata hivyo, NPS pia imetoa wito kwa umma kusaidia kufuatilia walipo watu waliopotea na kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika.