Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watu watatu akiwemo dereva bajaji, John Isaya (21) kwa tuhuma za kutengeneza na kusambaza picha mjongeo kwenye mitandao wa Tik Tok akitangaza kumuuza mtoto wake kwa Sh1.6 milioni.
Taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa Januari 6, 2024 na kusainiwa na Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, imeeleza kwamba Isaya ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Bukala wilayani Sengerema alifanya tukio hilo kutafuta umaarufu mitandaoni.
“Ukamataji wa mtuhumiwa huyo umetokana na taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi ambayo pamoja na taarifa hiyo ilieleza mtu huyo atafutwe, akamatwe ili aweze kuwajibika kisheria kwa kitendo alicho kifanya,” amesema Mutafungwa
Ameongeza kuwa,“ Ndipo Januari 4, 2025 saa 08:00 usiku katika Wilaya ya Sengerema Mkoa wa Mwanza tulifanikiwa kumkamata John Isaya. Chanzo cha tukio hill ni kutafuta umaarufu kupitia mitandao ya kijamii (Publicity),”
Amesema mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa kwa kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria na ni ukatili kwa mtoto huyo.
“Kitendo cha aina hii kama alivyofanya mtuhumiwa huyo kinaweza kusababisha madhara kwa watoto. Aidha, vitendo hivyo vinadhalilisha na kushusha thamani ya utu wa mtoto,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo linamshikilia Doto Maduhu Sita kwa tuhuma za kumbaka na kumlawiti mtoto wake wa kambo (1) pamoja na mama wa mtoto huyo, Aneth Sijaona (23) kwa kuficha tukio hilo
Mutafungwa amesema pamoja na kumfanyia ukatili huo, mkazi huyo wa Kishiri Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza pia alikuwa akimshambulia huku chanzo kikiwa ni tamaa ya ngono.
“Mtoto huyo alikuwa anafanyiwa ukatili huo mara kwa mara na kusababisha hali ya kiafya ya mtoto kuwa dhaifu na kuwafanya raia wema kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kupitia dawati la jinsia na watoto,
“Kutokana na taarifa hizo polisi walifika eneo la tukio hilo na kumkuta mtuhumiwa huyo akishirikiana na mke wake wakiwa katika jitihada za kumpeleka mtoto huyo ili apate tiba, walifika katika Kituo cha Afya cha Usumau kilichopo eneo la Kishiri,” amesema
Mutafungwa ameeleza kuwa baada ya kufika kituo hicho cha afya walielekezwa kumpeleka mtoto huyo Zahanati ya Serikali ya Igoma, hata hivyo mtoto huyo alifariki dunia Desemba 30, 2024 katika harakati za matibabu
“Pamoja na kumkamata mwanaume huyo pia tunamshikilia na kuendelea kumhoji mama mzazi wa mtoto huyo kwa kushindwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi au kwa jirani zake juu ya ukatili aliofanyiwa mtoto ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa na kuokoa maisha ya mtoto,” ameongeza
Amesema mwili wa mtoto huyo umefanyiwa uchunguzi na madaktari na tayari umekabidhiwa kwa baba mzazi wa mtoto huyo, Emmanuel Daud (28) na ndugu wengine kwa ajili ya mazishi.
“Uchunguzi kuhusiana na tukio hili unaendelea na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kuhusika katika ukatili huo ambao umesababisha kifo,” ameeleza Kamanda Mutafungwa.