RC Makongoro na mbio za kuwavuta wawekezaji sekta ya madini Rukwa

Rukwa. Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere amesema mkoa huo umeandaa mazingira rafiki na bora ili kuwavutia wawekezaji kuwekeza katika sekta ya madini.

Kauli hiyo ameitoa leo Jumanne Januari 7, 2025 alipokutana na kufanya mazungumza na wadau wa sekta ya madini mkoani humo.

Makongoro amesema kwa sasa Rukwa imekuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji kutokana na kufungua milango ya uwekezaji wa madini mbalimbali yanayopatikana mkoani humo.

Katika kikao kazi hicho, kilichomuhusisha pia Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi, Joseph Kumburu wadau kutoka kampuni za Trinity Southern Sahara Mining, Kidee Mining na wawekezaji watatu kutoka China, walioonesha nia ya kuwekeza kwenye sekta ya madini, hususani ya shaba.

Ofisa Madini Mkazi, Kumburu amesema Kampuni ya Trinity Southern Sahara Mining inamiliki leseni ndogo za uchimbaji wa madini ya shaba katika Kijiji cha Kirando na Itunya, Kata ya Kapalamsenga  na leseni ndogo ya uchimbaji wa dhahabu katika Kijiji cha Izinga, Wilaya ya Nkasi. “Na Kampuni ya Kidee Mining inamiliki leseni ya utafiti katika Kijiji cha Kirando na imeshawasilisha maombi ya leseni ndogo za uchimbaji wa dhahabu katika Kijiji cha Izinga,” amesema ofisa huyo.

Madini yanayopatikana katika maeneo tofauti ya mkoa wa Rukwa yakiwemo madini ya ulanga, shaba, emerald, titanium, dhahabu, helium, makaa ya mawe na aquamarine.

Katika mazungumzo yake na wadau hao, Makongoro amesisitiza kuwa Serikali ya Mkoa wa Rukwa imeweka mazingira bora na rafiki kwa wawekezaji katika sekta zote.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi, akiwamo Edson Mtavangu, mkazi wa Kijiji cha Mponda amesema Serikali kualika wawekezaji si jambo baya, bali wawekezaji hao watekeleze kile wanachokubaliana ikiwamo la huduma kwa wananchi.

Edson amesema kuna kasumba ya baadhi ya viongozi wa Serikali kuwapendelea wawekezaji huku wakisahau masilahi ya wachimbaji wadogo wa maeneo husika.

“Hapa kijijini tunachimba dhahabu, lakini linapokuja suala la mwekezaji, hatupewi kipaumbele, hasa sisi wazawa wa eneo hili,” amesema Edson.

Amesisitiza kuwa kuna haja ya Serikali kuhakikisha usawa kati ya wachimbaji wadogo wazawa, wawekezaji wa ndani na wa nje ili kuhakikisha kila upande unanufaika kwa haki.

Related Posts