Sababu wanafunzi kufeli masomo ya biashara, amali zatajwa

Dar es Salaam. Wadau wa elimu wameitaka Serikali kuongeza ajira za walimu wa masomo ya amali  ili kufikia lengo la kubadilisha mtalaa.

Ongezeko la walimu litasaidia wanafunzi kupata ujuzi stahiki utakaowasaidia kujiajiri watakapomaliza masomo na kupunguza idadi ya wanaofeli masomo hayo katika mitihani ya Taifa ya upimaji.

Wametoa maoni hayo wakati ambao matokeo ya mtihani wa upimaji kidato cha pili yaliyotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) yakionyesha kuwapo ufaulu hafifu katika baadhi ya masomo, likiwamo la kilimo ambalo asilimia 65.5 ya watahiniwa wanaolisoma walipata daraja F.

Masomo mengine ambayo wanafunzi walipata daraja F kwa wingi ni mazoezi ya viungo asilimia 74.76, uhandisi wa barabara (Civil Engineering Survey) asilimia 40.10, useremala na upakaji rangi (Woodwork and Painting Engineering) asilimia 40.8. Uchumi (Home Economics) asilimia 37.03, sayansi ya uhandisi (Engineering Science) asilimia 48.54.

Mbali na masomo haya ambayo huenda ndiyo mara ya kwanza kwa baadhi ya wanafunzi kujifunza, kwa yale ya biashara ambayo ni Commerce na Book-keeping waliopata F walikuwa asilimia 56.23 na asilimia 48.49 mtawalia.

Waliopata F katika masomo ya biashara ni ongezeko kutoka asilimia 49.72 na asilimia 47.16 iliyokuwapo katika mtihani wa upimaji kidato cha pili mwaka 2023.

Akizungumzia ufaulu huo, mdau wa elimu nchini, Muhanyi Nkoronko anasema kufeli kwa wanafunzi katika masomo hayo huenda kunasababishwa na kukosekana walimu.

Anasema ukosefu wa walimu unatokana na jambo linalofundishwa huenda likawa jipya au walimu waliokuwapo hawakuwa wengi kutosheleza kutoa maarifa stahiki kwa ajili ya kuwapa wanafunzi.

“Tunashindwa kuzalisha watu watakaoweza kujitegemea huko baadaye, kuwe na mpango wa kuongeza walimu watakaokuwa na uwezo wa kufundisha masomo hayo siku zijazo. Huenda waliopo wanamudu lakini ni wachache, hivyo haiwezekani kumfikia mwanafunzi mmojammoja,” anasema.

Nkoronko anasema ili kufanikisha hilo ni vyema Serikali ikaangalia namna ya kushirikiana na vyuo vya ualimu ili kuzalisha walimu wanaotakiwa kwa ajili ya kufundisha masomo yaliyopo.

Pia, kuangalia namna ya kuongeza vitabu vya kiada na ziada ambavyo vinaweza kuwasaidia wanafunzi kusoma waweze kupata maarifa mbalimbali.

“Kuwe na mkakati madhubuti wa Serikali kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo watunzi wa vitabu na taasisi ya kukuza mtalaa, waje na mpango kabambe wa kuandaa vitabu vya kutosha kwa ajili ya kukidhi mahitaji, jambo ambalo litakwenda sambamba na uboreshaji wa mbinu za ufundishaji kwa walimu waliopo,” anasema.

Hata hivyo, ushauri kuhusu kuajiri walimu ukitolewa, Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali katika kushughulikia ajira za walimu.

Imekuwa ikitangaza kutafuta walimu wa masomo ya amali kwa nyakati tofauti.

Mara ya mwisho ilikuwa Desemba 13, 2024, Serikali ilitangaza nafasi 3,633 za ajira za ualimu, huku nyingi zikiwa za masomo ya amali. Kada hizo zinarandana na matakwa ya Sera ya Elimu ya mwaka 2013 toleo jipya la mwaka 2023, ambalo limetoa kipaumbele katika elimu ya amali kama mbinu mojawapo ya kukabiliana na tatizo la ajira kwa wahitimu.

Nafasi zilitangazwa kupitia Sekretarieti ya Ajira, huku walimu waliokuwa wakihitajika kupitia tangazo hilo ni wa masomo ya biashara, ushonaji, uashi, umeme, ufundi magari, uchomeleaji na uundaji vyuma, sanaa, useremala, ufundi bomba, afya ya wanyama na uzalishaji chakula.

Wengine ni wa masomo ya kilimo na bustani, huduma ya chakula, upakaji rangi, umeme wa magari, jokofu na vipoza hewa, nishati ya jua, Tehama, uvuvi, usindikaji mbao na mazoezi ya viungo.

Mdau mwingine wa elimu, Nicodemus Shauri anasema kushindwa kufaulu kwa wanafunzi kunaweza kusababishwa na kuwapo walimu wasiotosheleza mahitaji.

Akizungumzia mapokeo ya wanafunzi katika masomo hayo, anasema wanasimama kama wanafunzi wa majaribio kwa kuanza kujifunza kitu kipya.

“Unajua katika ujifunzaji wanafunzi huwa wanatumia mitihani iliyopita kujifunza, sasa hawa kwa sababu ndiyo wa kwanza hakuna kitu cha nyuma wanachoweza kukisoma ili kuongeza uelewa na sidhani kama kuna vifaa vya kufundishia vinavyotosheleza,” anasema.

Katika kuboresha ufundishaji wa masomo hayo, Shauri anasema kila kitakachofanyika ni bora wanafunzi wapate ufaulu wa alama D kuliko F.

“Tuhakikishe walimu wanaajiriwa wa masomo hayo, vitabu vya kufundishia na kujifunzia vipatikane mashuleni na kama ni masomo ya amali tuhakikishe wanafunzi wanajifunza kwa vitendo,” anasema.

Anasema Serikali ishirikishe wadau wengine ili mabadiliko hayo yaweze kuleta matokeo yanayokusudiwa kufanyika. Wadau hao wataangalia ni maeneo gani wanayoweza kusaidia katika kuboresha mazingira ya ujifunzaji, huku Serikali ikiwawekea mazingira mazuri na wezeshi.

“Serikali na wadau pia wanapaswa kufanya tafiti katika nchi ambazo zinatekeleza mtalaa huu kuangalia ni njia gani zilitumiwa na zikawasaidia wao kutekeleza malengo waliyokuwa wamekusudia. Hii itatusaidia sisi kwani tutaweza kutumia uzoefu wa watu wengine,” anasema.

Related Posts