Serikali yaendelea na uchunguzi kesi ya ‘bwana harusi’ anayedaiwa kuiba gari

Dar es Salaam. Serikali imesema bado inaendelea na uchunguzi wa kesi ya mfanyabiashara Vicent Masawe (36) anayedaiwa kuiba gari lenye thamani ya Sh15 milioni.

Masawe aliyekuwa bwana harusi  anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni wizi wa gari aina ya Toyota Ractis alilodaiwa kuazimwa kwa ajili ya kulitumia katika sherehe ya harusi yake na kujipatia fedha taslimu Sh3 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Wakili wa Serikali, Titus Aaron ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumanne Januari 7, 2025, wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Wakili Aaron ametoa maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki kuwa, Serikali bado inaendelea na upelelezi wa shauri hilo, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Nyaki alikubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Februari 12, 2025 kwa ajili ya kutajwa.

Mshtakiwa Vicent Masawe (aliyevaa kofia) akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kesi ya wizi wa gari inayomkabili kuahirishwa leo Jumanne Januari 7, 2025. Picha na Hadija Jumanne

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 35738 ya mwaka 2024.

Katika kesi hiyo, mshtakiwa  ameshtakiwa chini ya kifungu 258 na 273(b) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Katika shtaka la kwanza, ni wizi wa kuaminika, Masawe anadaiwa kuwa, Novemba 15, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam, aliiba gari lenye namba za usajili T 642 EGU aina ya Toyota Ractis lenye thamani ya Sh 15milioni mali ya Silvester Masawe.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa, aliazimwa gari hilo  kwa lengo la kulitumia katika sherehe ya harusi yake, lakini baada ya hapo, hakurudisha gari kama ambavyo walikubaliana.

Shtaka la pili ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, tukio analodaiwa kulitenda Novemba 15, 2024 jijini Dar es Salaam.

Siku hiyo, mshtakiwa anadaiwa kwa lengo la kuiba na kutapeli, alijipatia Sh3 milioni kutoka kwa Silvester akidai atamrudisha fedha hizo baadaye, wakati akijua kuwa ni uongo na hakuweza kurudisha hadi alipokamatwa.

Kwa mara ya kwanza Masawe alifikishwa mahakamani hapo Desemba 24, 2024 na kusomewa mashtaka yanayowakabili.

Related Posts