Mlimba. Halmashauri ya Mlimba imeiweka katika uangalizi maalumu Shule ya Msingi Lugala iliyopo Kata ya Uchindile, Tarafa ya Mlimba wilayani Kilombero baada ya kufanya vibaya katika matokeo ya kitaifa ya darasa la nne kwa mwaka 2024.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa Januari 5, 2025, shule hiyo imepata wastani wa daraja F huku matokeo yakionesha hakuna mwanafunzi aliyepata daraja A wala B na daraja C amepata mwanafunzi mmoja, wengine sita wakiambulia daraja D na jumla ya waliofanya mtihani huo ni 30.
Mwananchi ilipomtafuta Ofisa Elimu Awali na Msingi wa halmashauri hiyo, Selina Fundi kuzungumzia suala hilo, alisema yuko safarini na angeweza kuzungumza akifika anapokwenda, lakini alipopigiwa tena, akasema yuko kikaoni.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Januari 7, 2025, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Jamal Abdul amesema kutokana na matokeo hayo wameona kuna haja ya kuiweka chini ya uangalizi maalumu shule hiyo kwa lengo la kutaka kudhibiti matokeo ya aina hiyo yasijirudie tena.
Abdul amesema kwa kuanzia timu ya viongozi ikiongozwa na ofisa elimu msingi wilaya, wadhibiti ubora elimu na viongozi wengine wa elimu wameshaenda shuleni hapo kwa lengo la kuchunguza chanzo cha matokeo hayo mabovu.
“Hata sisi, tumeshtushwa na matokeo haya, tayari timu imeenda shuleni hapo ili kuona tatizo ni nini na baada ya hapo, tutafanya uamuzi ambao utasaidia kurudisha hali ya shule hiyo,” amesema mkurugenzi huyo.
Aidha, amesema licha ya kusikiliza matatizo ya walimu na wanafunzi, watazungumza pia na uongozi wa kata kwa lengo la kudhibiti matokeo hayo yasijirudie huku akisisitiza kuwa huenda uongozi wa shule ukabadilishwa.
“Halmashauri hii inaongoza mara kwa mara kwa matokeo mbalimbali, ila shule hii kwa mwaka uliopita ndio imeiangusha na moja ya sababu iliyosababisha shule hii kufanya vibaya ni mahali pia ilipo, iko pembezoni mwa halmashauri, japo kuwa hii haiwezi kuwa sababu ya kutosha ya kufanya vibaya,” amesema Abdul.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Danstan Kyobya amesema timu ya wataalamu wa idara ya elimu wakiongizwa na mkurugenzi wa halmashauri, wameanza kufanyia kazi tatizo hilo.
“Tukishajua sababu, sisi kama Serikali ndio tutajua tuanzie wapi, kimsingi matokeo haya yametuumiza na lazima hii shule tuitupie jicho la kipekee na tuifuatilie kwa karibu kwa kuweka mikakati mahususi ya kuikomboa kwenye matokeo haya mabovu, licha ya kuwa mbali, lakini lazima tuelekeze nguvu kubwa huko,” amesema Kyobya.