Sura tofauti za mnyukano wa Gambo, Makonda

Dar es Salaam. Ingawa majibizano baina ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, na Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo, yanatafsiriwa kuwa hulka za viongozi hao, wanazuoni wanayahusisha na vikumbo kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Kwa mujibu wa wanazuoni waliobobea katika sayansi ya siasa, kilichojificha nyuma ya majibizano au ugomvi, kama inavyodaiwa na wengi, kinaibua maswali lukuki.

Mitazamo hiyo ya wasomi inatokana na kilichotokea jana, Jumatatu, Januari 6, 2025, kati ya Gambo na Makonda, baada ya mbunge huyo kuwasilisha ombi la kujengwa barabara ya kona ya Kiseria, Mushono, itakayounganisha na Bypass ili kupunguza foleni kuelekea kwenye mashindano ya Afcon 2027.

Kwa mujibu wa Gambo, katika barabara hiyo Tanroads imejenga kilomita moja na mwaka huu wa fedha haikutengewa bajeti, licha ya kupelekwa maombi maalumu na kuahidiwa kwamba itatekelezwa.

“Ombi langu jingine ni barabara ya Arusha Kibaya hadi Kongwa, ambayo Jiji la Arusha tungepata kilomita 27, lakini toka mwaka 2022 hatujamuona mkandarasi. Ningependa utumie fursa hii utueleze zile kilomita 27 kwa ajili ya Afcon Serikali ina mpango gani wa kuziweka vizuri,” alisema Gambo.

Alipopokea kipaza sauti, Makonda alisema maombi yanayotolewa na mbunge huyo ni kwa sababu hahudhurii vikao, kwani yalishajadiliwa vikaoni, akisisitiza anachokifanya ni utovu wa nidhamu.

“Nimsaidie Waziri (Ulega). Hoja alizozisema Gambo kwenye vikao haji. Ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu kumsubiri kiongozi kwenye hadhara ili umvie upachike mambo,” alisema Makonda.

Ukiachana na hilo, kumekuwa na historia ya misuguano kati ya Gambo na viongozi mbalimbali aliowahi kufanya nao kazi, tangu alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Januari 2019, Gambo aliingia kwenye ugomvi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro. Kipande cha picha jongefu kiliwaonyesha wakitupiana maneno kuhusu suala la mabati katika Kituo cha Afya Murieti.

Mzizi wa ugomvi huo ulikuwa wasiwasi ulioonyeshwa kuhusu kiwango cha mabati yaliyotumika katika ujenzi wa kituo hicho cha afya, ambayo ni geji 30 badala ya 28 inayotakiwa na Serikali.

Ugomvi mwingine uliomhusu Gambo ulikuwa dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk Maulid Madeni, akimtuhumu kwa kupeleka maneno kwa wakuu wake na hivyo kumharibia.

Katika kipande kingine cha picha jongefu, Novemba 2019, Gambo alionekana akimsema Dk Madeni akimwambia: “Msemaji wa mkoa huu ni Mkuu wa Mkoa na halmashauri zote zipo chini ya Mkuu wa Mkoa. Hakuna anayeweza kuwa na kauli zaidi ya Mkuu wa Mkoa.”

Kwa upande wa Makonda, Septemba 25, 2019 akiwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, katika moja ya mkutano wake na wakuu wa wilaya, aliwahi kumfokea aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo akimtaka akae kimya, baada ya kujaribu kufafanua maswali yaliyoulizwa na Makonda.

 “Wee… kaa kimya.. kaa kimya. Hakuna mtumishi ambaye yuko juu ya hili, hatufurahii ujinga hapa hakuna mtumishi aliye juu ya Katibu Tawala wa Mkoa, mtumishi yeyote anayejua wajibu wake anajua nafasi ya RAS,” alisema Makonda.

Pia Mei, mwaka 2017 Makonda alitishia kuwachapa viboko watumishi wa umma, iwapo wangebeba mabango katika sherehe za Mei mosi, kushinikiza nyongeza ya mshahara.

“Ningewaona sijui jumangapi ile tarehe moja, Mei mosi mmebeba mabango eti, bila kuongeza mshahara hii kauli ya hapa kazi tu ningewachapa viboko wala msingeamini,” alisema.

Kabla ya ugomvi na watendaji wenzake ndani ya Serikali, Gambo aliwahi kuwa na tofauti na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.

Ugomvi wao ulikolezwa Oktoba 18, 2016, baada ya Gambo kusema mradi wa jengo la mama na mtoto Burka mkoani humo ulitokana na maono ya Nyaga Mawala.

Kauli hiyo ilisababisha Lema asimame hapohapo kumpinga Gambo na kueleza kuwa yeye ndiye aliyehusika kutafuta ardhi na wafadhili, na kwamba maelezo ya awali yamejaa upotoshwaji na siasa.

Mei 2022, Gambo alimtuhumu aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kenani Kihongosi, na watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kujihusisha na vitendo vya rushwa mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Tuhuma hizo zilisababisha kusimamishwa kazi kwa watendaji sita wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji, Dk John Pima. Wote hao, Gambo aliwatuhumu kujiingizia fedha za halmashauri katika akaunti zao binafsi, huku Kihongosi akidaiwa kupokea mgawo wa Sh2 milioni kupitia akaunti ya mkewe.

Hilo lilikwenda mbali zaidi, hadi Waziri Mkuu akamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi huo, huku Dk Pima na wenzake wakiwekwa kando.

Baadaye, Dk Pima na wenzake walishitakiwa mahakamani, wakahukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kisha wakashinda rufaa na kuachiwa huru.

Haikuishia hapo. Mienendo ya ugomvi wa Gambo dhidi ya viongozi wengine, Juni 2024, ilisababisha Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa, amtaje kuwa kikwazo cha kukamilika kwa miradi ya maendeleo.

Alisema mbunge amekuwa akiingia katika migogoro na wataalamu wa halmashauri na madiwani, jambo lililojibiwa na Gambo kuwa si kweli, bali Mtahengerwa mwenyewe ameshindwa kuwasimamia watendaji wake.

Mtahengerwa pia, Aprili 2024, aliwahi kumtaka Gambo aache kile alichokiita siasa za maji taka, baada ya kulituhumu Jiji la Arusha kuhusika na ufisadi katika miradi ya maendeleo.

Kauli hiyo ya Mtahengerwa ilitokana na hoja iliyoibuliwa bungeni na Gambo, akiutuhumu uongozi wa jiji hilo kuhusika na ufisadi katika miradi mbalimbali.

Hata hivyo, Machi mwaka jana, Gambo alisema kinachodaiwa kuwa ugomvi wake na watendaji mbalimbali kinatokana na msimamo wake wa kusimamia makubaliano. Sambamba na hilo, Gambo alidai kuwepo kwa viongozi wanaowahujumu wale wanaochaguliwa na wananchi kwa kubadilisha makubaliano ya bajeti katika jimbo hilo.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo, amejenga hoja yake kwa maswali anayosema watu wanapaswa kujiuliza kabla ya kumlaumu yeyote.

Hata hivyo, ameelekeza majibu yake kwa tukio la hivi karibuni kati ya Gambo na Makonda. Miongoni mwa maswali hayo ni: Kabla ya Makonda, Gambo alikuwa anagombana na Mkuu wa Mkoa aliyekuwepo (John Mongela).

Swali lingine amehoji ni: Gambo, tangu alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha na baadaye Mbunge, ana historia ya kudanganya na kutohudhuria vikao?

Ukiachana na maswali kuhusu Gambo, Dk Masabo amesema pia watu wajiulize historia ya uhusiano wa Makonda na wabunge katika mkoa aliouongoza (Dar es Salaam) kabla ya Arusha.

Maswali hayo, mwanazuoni huyo amesema, yatatoa jawabu la ama ugomvi ni hulka ya viongozi hao au vinginevyo, huku akigusia kuwa nyakati za kuelekea uchaguzi kupigana vikumbo ni jambo la kawaida.

“Sijaona kosa la Gambo katika kuuliza lile jambo hadharani na sielewi kwanini Mkuu wa Mkoa (Makonda) ameamua kumshambulia. Ile alikuwa anampa nafasi Waziri kueleza mbele ya wananchi kwa mdomo wake, sio mambo yabaki vikaoni,” amesema.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe, amesema kilichoshuhudiwa ni misuguano ya kawaida kwa vijana kwenye mamlaka.

Ameeleza kabla ya kurudi katika historia za wawili hao, ni vema kujua Gambo na Makonda ni vijana na damu zinachemka, ingawa jambo la busara ni kila upande ujue mipaka yake na kuheshimiana.

“Misuguano kama hii haina tija kwa wananchi. Wananchi wanataka maendeleo na kuona matokeo ya kazi ama ya mbunge au Mkuu wa Mkoa. Mikwaruzano baina ya pande mbili haiwanufaishi chochote wananchi,” amesema.

Hata hivyo, msomi huyo amesema kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi, mengi yatasikika na dhamira yake ni kujiweka mbele kisiasa.

Related Posts