TANZANIA KUSHIRIKIANA NA ITALIA KUENDELEZA SEKTA YA MADINI

▪️Mkutano wa Wafanyabiashara wa Tanzania na Italia kufanyika Mwezi Februari, 2025.

▪️Kampuni za Utengenezaji Vifaa kutoka vya Madini kutoka Italia kushiriki.

▪️Wachimbaji kunufaika na teknolojia na mitambo rafiki kwa mazingira

Dar es Salaam

Waziri wa Madini, Mh. Anthony Mavunde (Mb) amesena kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na Italia katika kuendeleza sekta ya madini nchini hususani katika teknolojia na mitambo.

Ameyasema hayo jana tarehe 06 Januari, 2025 alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mh. Giuseppe Coppola katika ofisi ndogo za Wizara ya Madini Jijini Dar es Salaam.

“Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameifungua nchi yetu kwa kuimarisha mahusiano kimataifa kupitia falsafa yake ya 4R. Sisi wasaidizi wake tutaendelea kuhakikisha tunasimamia maono hayo na kujenga mahusiano zaidi na washirika wetu kwa manufaa ya uchumi na wananchi wa pande zote.

Zipo fursa nyingi kwenye sekta ya madini nchini kuanzia kwenye utafiti mpaka uongezaji thamani madini, mazingira ya uwekezaji ni mazuri hivyo ninawakaribisha sana wawekezaji kutoka nchini Italia kuja kuwekeza Tanzania“alisema Mavunde.

Kwa upande wake Balozi Coppola, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano inaompa tangu awasili nchini, na kusisitiza kwamba Italia inayo makampuni mengi ambayo yamejikita katika teknolojia hususan utengenezaji wa mitambo inayotumika kwenye sekta ya madini.

“Mwezi Februari, 2025 tunataraji kuwa na mkutano wa wafanyabiashara baina ya Tanzania na Italia ambapo tunatarajia makampuni na wawekezaji katika sekta zote hususan madini kuja kushiriki mkutano huo. Ninaamini kwa kutumia mkutano huo utakuwa ni mwanzo mzuri wa wawekezaji kutoka Italia kuona fursa zilizopo nchini Tanzania na kuanza kuzichangamkia” alisisitiza Mhe. Coppola.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde alionesha kufurahishwa na mpango wa mkutano wa wafanyabiashara wa Italia na Tanzania na kutanabaisha kwamba ni vizuri taarifa za kina kuhusu mkutano huo zikaifikia Wizara mapema kwa ajili ya uratibu ili wachimbaji wakubwa na wadogo waweze kushiriki kikamilifu na kuleta tija.




Related Posts