Sichuan. Tetemeko la ardhi lililolikumba Jimbo la Dingri katika Mkoa wa Tibet nchini China limesababisha vifo vya watu 125 huku 188 wakijeruhiwa.
Televisheni ya Taifa ya China (CCTV) imeripoti kuwa, tetemeko hilo lenye mtikisiko wa 7.1 limelikumba jimbo hilo leo Jumanne Januari 7, 2024 kuanzia Saa 3:05 asubuhi.
Taarifa hiyo imesema kuwa Taasisi ya Usimamizi wa Matetemeko nchini China imetangaza hali ya dharura na kutuma watoa huduma za dharura maeneo yote yaliyoguswa na tetemeko hilo.
Watoa huduma ya uokoaji wanaendelea kuwatafuta watu walionasa kwenye vifusi baada ya tetekemeko hilo kuharibu majengo zaidi ya 1,000, mengine yanatajwa kuporomoka hususan ni eneo la Tibet, karibu na Mlima Everest.
Kutokana na janga hilo, Rais wa China, Xi Jinping ametangaza hali ya dharura huku akiagiza kufanyika kwa uokoaji kila mahali palipoguswa na tetemeko hilo sambamba na kufuatilia athari zake kwa Umma.
Kwa mujibu wa CCTV, tetemeko hilo lilianzia katika ukingo wa milima ya Himalaya huku hali ikitajwa kuwa mbaya zaidi kutokana na hali ya hewa nchini kuwa baridi inayodhaniwa kufikia hadi nyuzijoto-16 (3.2F) inapofika usiku.
Televisheni hiyo imeripoti kuwa matetemeko ya ardhi hutokea mara kwa mara katika ukanda huo unaoegemea katika mchaniko wa kijiografia japo tetemeko la leo ni kubwa kuliko matetemeko yaliyowahi kutokea eneo hilo.
Wakati linatokea, tetemeko hilo lilitikisa na kuathiri eneo lenye upana wa Kilometa 10 (maili sita).
Takwimu hizo zimetolewa na Kituo cha Utafiti wa Miamba nchini Marekani, huku kikisema athari zake zimeeenea hadi nchini Nepal na sehemu ya Taifa la India linalopakana na Tibet.
Vipande vya video vilivyorushwa na CCTV, vinaonyesha majengo yakiwa yameporomoka hususan ni Mji wa Shigatse, huku waokoaji wakipambana kutoa vifusi na mablanketi ya wamiliki wa majengo hayo.
Mmiliki wa Duka la Jumla lililoathiriwa na tetemeko hilo, Sangji Dangzhi, amesema athari zake ni kubwa katika bidhaa na mali iliyokuwa ndani ya duka lake.
“Majengo mengi hapa yamejengwa kwa udongo kwa hiyo lilipotokea tetemeko… majengo mengi yameporomoka,” amesema Sangji.
Ameongeza kuwa magari ya kubeba wagonjwa yanaendelea kusomba watu walioathiriwa na janga hilo.
Mgeni katika moja ya Hoteli eneo la Shigatse alikieleza chombo cha habari cha Fengmian News kuwa alishtushwa na mtikisiko wa tetemeko hilo alipokuwa amelala.
Anasema baada ya kushtuka alichokumbuka kubeba ni soksi zake ili asidhurike miguu yake kutokana na baridi kali inayoendelea kulikumba eneo hilo na kukimbilia eneo la wazi.
“Nilihisi kama ni kitanda kimenyanyuliwa ghafla kiasi kwamba hofu ikanijaa,” amesema.
Amedokeza kuwa, huenda tetemeko hilo limeanzia Tibet kwa kile alichodai eneo hilo limekuwa likikumbwa na matetemeko madogo kila mara.
Mifumo ya maji na Umeme imeathiriwa mkoani humo.
Kwa mujibu wa mtafiti kutoka Kituo cha Matetemeko nchini China (CENC) Jiang Haikun, ameieleza CCTV kuwa tetemeko lingine lenye ukubwa wa 5.0 linaweza kutokea wakati wowote kuanzia sasa katika eneo hilo huku akisema tetemeko hilo litakuwa na madhara machache kulinganisha na lililotokea asubuhi ya leo.
Tayari, Vituo vya watalii wa kukwea mlima Everest eneo la Tingri, vimesitisha huduma hiyo kuanzia leo asubuhi, kwa sababu za kiusalama.
Mkoa wa Shigatse, unaokadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya 800,000 ndipo yalipo makazi ya Panchen Lama, ambaye ni mrithi wa kiongozi wa dini Kibudha (Tibetan Buddhism) Dalai Lama.
Kiongozi huyo ya kiroho anayeishi uhamishoni ameieleza BBC kuwa ameshtushwa na tukio hilo.
“Ninawaombea wote waliofariki na waliopoteza wapendwa wao na ninawatakia majeruhi hali ya kupona haraka,” amesema kiongozi huyo wa kiroho.
Kikosi cha Anga cha China pia kimeanzisha Operesheni yake maalum ya kuokoa waliofukiwa na vifusi kwa kusambaza droni katika maeneo yaliyoathiriwa na janga hilo.
Mwaka 2015, tetemeko la aina hiyo lenye ukubwa wa 7.8 liliukumba Mji wa Mkuu wa Nepal, Kathmandu, na kuua zaidi ya watu 9,000, huku zaidi ya 20,000 wakijeruhiwa.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.