KOCHA Mkuu wa Alliance Girls, Sultan Juma amesema kwa sasa Simba Queens na JKT Queens hazina upinzani kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake kutokana na kufanya usajili bora na uwekezaji mkubwa.
Ligi hiyo ambayo imemaliza mzunguko wa kwanza, mabingwa watetezi, Simba Queens wako kileleni na alama 25 wakishinda nane na sare moja wakiwa hawajapoteza mechi yoyote kati ya tisa walizocheza, huku JKT Queens iliyocheza mechi nane ikiwa na pointi 20. Mashujaa Queens iliyo kwenye nafasi ya tatu ina alama 15.
Tangu mwaka 2016 ligi hiyo ilipoasisiwa, timu tofauti iliyobeba ubingwa wa michuano hiyo nje ya Simba Queens na JKT Queens ni Mlandizi Queens pekee iliyochukua mwaka 2016, huku timu hizo mbili zikipishana misimu mingine.
Juma aliliambia Mwanaspoti kuwa kwa sasa hali ilivyo timu nyingine nane zinapaswa kuusahau ubingwa na zishindanie nafasi nne.
“Kwenye ubingwa kuna farasi wawili, hakuna timu yoyote ambayo itasema kwamba inataka ubingwa, hao wawili ndiyo wanashindana na inaeleweka ligi yetu wanapishana tu wale farasi wawili sisi wengine tunaangalia hizo nafasi nne, tunasema kila wakati kwamba uwekezaji na usajili watu wanafanya usajili mzuri kwa hiyo kuna wakati usiwe muongo uongee uhalisia. Tulivyosajili na walivyosajili wao ni tofauti hata uwekezaji wao na wetu havifanani, wachezaji wetu ni wanafunzi wachache ndiyo wanatoka nyumbani.”€
Kocha huyo wa zamani wa Geita Gold Queens alisisitiza kuwa: “Kusema tunawania ubingwa nitakuwa nawaongopea watu, nasema ukweli ili niwe salama, hiyo nafasi ya ubingwa siioni kwa sababu uwekezaji na usajili tuliofanya, JKT na Simba.”