ILE Ligi ya Kikapu Daraja la Kwanza Mkoa wa Dar es Salaam imeendelea kushika kasi katika Uwanja wa Bandari, Kurasini, ambapo timu mbalimbali zinaendelea kuonyeshana ubabe zikiwania kupanda daraja.
Katika michezo hiyo, Stein Warriors iliendelea kuonyesha makali baada ya kuifunga Mbezi Beach kwa pointi 61-45.
Mchezo huo ulioshuhudiwa na watazamaji wengi katika Uwanja wa Bandari Kurasini, ulishuhudia Stein Warriors inashika nafasi ya pili katika ligi hiyo kwa pointi 27, huku nafasi ya kwanza ikiangukia mikononi mwa Polisi yenye pointi 28.
Katika mchezo dhidi ya Mbezi Beach, Stein warriors iliongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 12-8, ile ya pili 26-14 na hadi kufikia mapumziko washindi hao walikuwa wanaongoza kwa pointi 38-22.
Mbezi Beach ilizinduka katika robo ya tatu na kufanikiwa kufunga pointi 12-13, huku Stein Warriors ikipata pointi 13-11 katika robo ya nne.
Katika mchezo huo, James Ngaboyeka wa Stein Warriors alifunga pointi 18 akifuatiwa na Davis Mshamu aliyefunga pointi 17, ilihali upande wa Mbezi Beach alikuwa ni Adam Ramadhani aliyefunga pointi 17 akifuatiwa na Jackson Mrisho aliyefunga pointi 16.
Katika mchezo huo kikundi cha muziki cha Stein Warriors kilivutia mashabiki wengi wa kikapu waliofika kuangalia mchezo huo.
Kivutio kikubwa kilitokana na jinsi wanavyokuwa wasanii wa kikundi hicho walivyokuwa wakicheza muda wote wa mchezo wakati timuhiyo ikicheza katika kutoa hamasa kwa wachezaji.
Kupitia onyesho hilo uwanja ulifurika wakazi wengi wa maeneo ya Bandari kuangalia mchezo huo.
Katika mchezo mwingine, pointi 35 zilizofungwa na Premier Academy katika robo ya tatu na ya nne zilichangia kwa timu hiyo kuifunga Donbosco VTC kwa pointi 61-48 katika ligi hiyo.
Premier Academy iliyoanza kinyonge katika robo ya kwanza na pili ikifungwa pointi 15-12, 15-14 ilibadilika katika robo ya tatu na ya nne.
Katika robo ya tatu ilifunga pointi 14-6 na ile ya nne ikapata pointi 21-12.
Katika mchezo huo, Calvin Mushi alifunga pointi 23 akifuatiwa na Diocres Mugaya pointi 19, huku upande wa Donbosco VTC akiwa ni Junior Ngowo aliyefunga pointi 17 ilhali Peter Bazar akifunga 16.
Mechi nyingine iliyopigwa uwanjani hapo ilishuhudia dakika tano za nyongeza zikiiwezesha PTW kuifunga Mlimani BC kwa pointi 74-66.
Kabla ya dakika hizo kuongezwa, timu hizo zilikuwa zimefungana pointi 62-62.
PTW inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania iliongoza katika robo ya kwanza na ya pili kwa pointi 13-10 na 27-20, huku ile ya tatu Mlimani BC ikiongoza kwa pointi 11-6 na ya nne ikapata pointi 21-16 na matokeo kuwa 62-62.
Ndipo sheria ilitumika ya kutafuta mshindi zikaongezwa dakika tano na katika muda huo PTW ilifunga pointi 12-4 na kufanya timu hiyo iibuke na ushindi wa pointi 74-66.
Katika mchezo huo Justine Ngindo alifunga pointi 20 akifuatiwa na Niaka Kienda aliyefunga 15, huku Baraka Kweka akiifungia Mlimani BC alama 16 ilhali Shalom Mwakyosi akifunga 10.
DAR KINGS YAIBURUZA MAGNET
Nayo Dar Kings iliifumua Magnet kwa pointi 72-48 katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza.
Ushindi ilioupata timu hiyo unafuatia ule wa Jumamosi iliyopita dhidi ya timu Donbosco VTC wa pointi 48-47.
Dar Kings ilianza mchezo katika robo ya kwanza ikionyesha dhamira ya ushindi kutokana na upungufu wa wapinzani wake.
Upungufu huo ulitokana na timu hiyo kuwa na idadi ndogo ya wachezaji wakiwa ni watano bila kuwapo wa akiba.
Katika mchezo huo, Dar Kings iliongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 30-8, 15-15 na hadi kufikia mapumziko washindi walikuwa wanaongoza kwa pointi 35-23.
Katika robo ya pili iliongoza tena kwa pointi 14-9, huku Magnet ikipata pointi 16-13 katika robo ya nne.