Arusha. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Geita, imewaachia huru watu 10 wakiwamo wa familia moja waliokuwa wakishtakiwa kwa kesi ya mauaji ya wanandoa.
Mauaji hayo yanadaiwa kusababishwa na mgogoro wa muda mrefu wa mirathi kuhusu shamba la familia la ekari 400.
Waliokuwa wakishtakiwa ni Ernests Nyororo, Zanzibar Madegeleki, Lucas Madegeleki, Lushingi Madegeleki, Kesi Madegeleki, Simon Madegeleki, Kinyonga Madegeleki, Jumanne Makaranga, Tulo Kisasembe na Mpina Madegeleki.
Watu hao walishtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, wakidaiwa kuwaua Japhet Nyororo aliyekuwa msimamizi wa mirathi na mkewe Winfrida Kabwata.
Ilidaiwa kuwa, watuhumiwa walitenda kosa hilo Januari 2, 2024, katika Kijiji cha Ihanga Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita.
Japhet (marehemu), alidaiwa kuuza sehemu ya ardhi bila ridhaa ya wanafamilia wengine, jambo lililodaiwa kuzua chuki miongoni mwa wanandugu hao.
Kesi hiyo iliyosikilizwa na Jaji Griffin Mwakapeje, alitoa hukumu hiyo Jumatatu Januari 6, 2025, baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kupitia vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo.
Katika hukumu yake ambayo nakala yake inapatikana kwenye mtandao wa Mahakama, Jaji Mwakapeje alisema Mahakama imewaachia huru washitakiwa hao baada ya kuwakuta hawana hatia kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa moja kwa moja unaowaunganisha na mauaji hayo.
Jaji alibainisha kuwa, upande wa mashtaka haukutimiza wajibu wake wa kuthibitisha mashtaka ya mauaji bila kuacha shaka, hasa ikizingatiwa kuwa kesi hiyo ilitegemea ushahidi wa kimazingira.
Upande wa mashtaka, uliokuwa na mashahidi 18 na vielelezo vinne, uliwakilishwa na mawakili wa Serikali watatu wakiongozwa na Godfrey Odupoy, huku washtakiwa wakitetewa na mawakili tisa.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, washtakiwa wote 10 walikana kuhusika na mauaji hayo na ushiriki wowote katika mikutano ikiwamo ya kuchangisha fedha, huku baadhi ya washtakiwa wakidai kutofahamu mgogoro wa ardhi na mirathi hiyo.
Shahidi wa kwanza wa Jamhuri, ambaye ni mtoto wa marehemu hao, Anastazia Japhet alidai kuwa, usiku wa Januari 2, 2024 akiwa nyumbani, alisikia kelele nje na kuwaona watu watano wenye silaha wakimshambulia baba yake.
Amedai kuwa, alijifungia ndani ya nyumba, lakini baadaye alipotoka, alikuta wazazi wake wote wameuawa.
Anastazia amedai kuwa, alilazimika kupiga kelele kuomba msaada polisi ambao walifika, kuchukua taarifa za awali na miili ya marehemu.
Anastazia amedai kulikuwa na mgogoro wa ardhi baina ya baba yake na mjomba wake (mshtakiwa wa kwanza), lakini hakuweza kuwatambua waliowaua wazazi wake au kuunganisha moja kwa moja mauaji hayo na mgogoro huo.
Shahidi wa pili ambaye ni mganga wa kienyeji, Nanyige Shija (80) kutoka Kijiji cha Kangabuka, amedai kuwa, Januari 3, 2024 watu wawili walikiri kwake kumuua mwanamume na mwanamke kwa sababu ya ugomvi wa ardhi na kumuomba msaada wa kujisafisha.
Amedai awali alikataa, lakini alitekeleza matambiko hayo waliporudi na watu wengine sita.
Hata hivyo, amedai hakuwatambua watu hao kutokana na kutoona vizuri usiku na alithibitisha kutekeleza matambiko hayo kwa malipo.
Shahidi wa saba, Dk Philimon Mtunya akizungumza mahakamani hapo, amesema Januari 3, 2024 alifanya uchunguzi wa miili miwili iliyofikishwa katika Kituo cha Afya Bwanga.
Katika ushahidi wake, Dk Mtunya alidai kifo cha Japhet kilisababishwa na kutokwa damu nyingi katika majeraha makubwa aliyokuwa nayo kichwani.
“Mheshimiwa jaji, kuhusu Winfrida, kifo chake pia kilisababishwa na kutokwa damu nyingi kutokana na jeraha kubwa alilokuwa nalo kichwani pia liliharibu ubongo na alikuwa na jeraha lingine kwenye mkono,” amedai shahidi huyo.
Shahidi wa 15, Hakimu Mkazi Mfawidhi Yahya Yassin amedai kuwa, Januari 10, 2024 alirekodi maelezo ya mshitakiwa Zanzibar aliyekiri kuhusika katika mauaji hayo, yakihusishwa na mgogoro wa ardhi ya familia.
Amesema Januari 23, 2024 alirekodi maelezo ya Lucas, ambaye pia alikiri kuhusika, akielezea mpango ulioratibiwa na Ernest pamoja na ushiriki wa ndugu wengine.
Shahidi wa 16, ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi, Winfrida Mrosso alitoa ushahidi wake na kudai kurekodi maelezo ya Tulo na Mpina, waliokiri kushiriki mauaji hayo.
Baada ya kesi kufungwa, washtakiwa wote 10 walipatikana na kesi ya kujibu na kila mmoja alitoa utetezi wake chini ya kiapo na kukana kuhusika na makosa ya mauaji yanayowakabili.
Mshtakiwa wa kwanza, Ernest, katika utetezi wake, aliiambia Mahakama kuwa shamba la familia 400 liligawanywa mwaka 2015 baada ya kifo cha mjomba wake aliyemtaja kwa jina la Madegeleki Nyororo.
“Na mwaka 2018, Japhet aliteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi na mwaka 2019 ardhi hiyo iligawanywa rasmi,” amedai.
Hivyo, Ernest aliiambia Mahakama kuwa katika mgawanyo wa mirathi hiyo, alipokea Sh1 milioni kwa kuuza sehemu ya eneo lake alilogawiwa na akasisitiza kutohusika na mauaji hayo.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, Jaji Mwakapeje alianza kwa kufafanua kanuni zinazoongoza kesi za jinai, akieleza ni jukumu la upande wa mashtaka kuthibitisha kesi bila kuacha shaka yoyote.
Jaji Mwakapeje amesema kwa kuzingatia ushahidi wa upande wa mashtaka uliopo, washtakiwa wote wanahusishwa na mauaji ya marehemu kupitia ushahidi wa kimazingira.
Hata hivyo, amebainisha kuwa, hakuna shahidi wa upande wa mashtaka aliyethibitisha kuwaona washtakiwa wakipanga au kutekeleza mauaji hayo.
“Katika kesi za jinai, ushahidi wa kimazingira unatumiwa kumtia mtu hatiani. Mahakama lazima ijiridhishe kwamba ushahidi huo, ukiunganishwa pamoja, hauleti hitimisho jingine la maana zaidi ya hatia ya mshtakiwa. Ushahidi huo, lazima utengeneze mlolongo wa hali unaoendana na hatia ya mtuhumiwa,” amesema Jaji huyo.
Pia, amesema ni jambo lisilopingika kuwa upande wa mashtaka ulijikita katika madai kwamba, marehemu Japhet na mkewe waliuawa kutokana na migogoro ya urithi wa ardhi ya familia.
Amesema ilithibitishwa kuwa, vikao vya mpango vilifanyika katika ukoo wa Nyororo na kila mjumbe alitakiwa kutoa Sh100,000 kwa ajili ya kuajiri watu binafsi kutekeleza mauaji hayo. Hata hivyo, hakuna shahidi yeyote wa mashtaka aliyethibitisha kuhudhuria mikutano hiyo au kueleza jinsi michango hiyo ilivyokusanywa.
Jaji Mwakapeje amesema kutokana na kesi hiyo kutegemea ushahidi wa kimazingira, Mahakama iliona kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuweka uhusiano wa moja kwa moja kati ya ushahidi uliotolewa na ushiriki wa washtakiwa katika kutekeleza mauaji hayo kama walivyoshitakiwa.
“Hakuna ushahidi wa kuaminika unaoonyesha kuwa, mauaji hayo yalitokana na mgogoro wa ardhi kati ya watuhumiwa na marehemu. Baadhi ya ushahidi huo unaibua shaka na haukidhi kiwango kinachohitajika kisheria, kuwataja watuhumiwa kama wahusika wa mauaji ya Japhet na Winfrida.
“Kwa msingi huo, ninaona kuwa, washtakiwa hawana hatia ya kosa la mauaji kama walivyoshitakiwa. Kwa kuzingatia hayo, ninawaachia huru washtakiwa wote 10,” amehitimisha Jaji Mwakapeje.