Dar es Salaam. Katika jitihada ya kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwamo rushwa ya ngono kwa wanawake wajasiriamali, taasisi inayoshughulika na uwezeshaji wa wasichana ya Her Initiative imekuja na jukwaa mseto la kidigitali la Ongea Hub ili wasichana wajasiriamali waripoti matukio ya ukatili wa kijinsia.
Pia, kupitia jukwaa hilo wasichana wajasiriamali wanaunganishwa na mamlaka zinazotoa msaada wa kisheria, kisaikolojia, kihisia na kijamii kwa kutumia tovuti na mfumo wa akili bandia kupitia ujumbe mfupi (SMS).
Ongea Hub ni sehemu ya jukwaa la Panda Chat linalounganisha wajasiriamali na wataalamu mbalimbali katika eneo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 7, 2025, Mkurugenzi mwanzilishi wa Her Initiative, Lydia Charles amesema kuwa baadhi ya wasichana katika shughuli zao za kiuchumi wamekuwa wakikumbana na changamoto za ukatili wa kijinsia ikiwamo rushwa ya ngono, jambo linalorudisha nyuma jitihada zao.
Lydia amesema baadhi ya waathirika kutokana na hofu pamoja na kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu haki zao, wamejikuta wakishindwa kuripoti matukio hayo kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe.
“Hili linachochea vitendo hivyo kuendelea kujitokeza katika jamii jambo ambalo linarudisha nyuma jitihada zinazofanywa na wadau mbalimbali katika kukomesha vitendo hivyo,” amesema.
Amesema ili kuondoa changamoto hiyo sasa waathirika wa vitendo hivyo vya ukatili ikiwamo rushwa ya ngono kupitia simu zao wanaweza kuripoti matukio hayo na kupatiwa msaada kutoka kwa wataalamu, mbalimbali kulingana na mahitaji yake.
“Kupinga rushwa ya ngono na ukatili si jukumu la mtu mmoja, ni harakati ya pamoja, jukwaa hilo linalotuunganisha sote katika kujenga mazingira salama kwa wanawake wajasiriamali kuweza kuuliza maswali magumu kuhusu ukatili wa kijinsia na kupata majibu yake,” amesema.
Ameeleza kuwa, jukwaa hilo pia ni sehemu ya uzinduzi wa kampeni yao ya ‘Haki Haiuzwi’ ambayo inalenga kutengeneza vinara wa kupinga rushwa ya ngono miongoni mwa wasichana wajasiriamali.
“Kupitia kampeni hiyo wasichana hao vinara watapita katika masoko mbalimbali ya wajasiriamali, kutoa elimu kuhusu haki na wajibu wao pamoja na masuala yote yanayohusiana na ukatili wa kijinsia,” amesema Charles.
Ameongeza kuwa kupitia jukwaa hilo pia wajasiriamali hao wanaweza kupata msaada kuhusu changamoto mbalimbali za kibiashara wanazokutana nazo kutoka kwa wataalam mbalimbali katika eneo hilo kupitia simu zao za mkononi.
“Elimu, pekee haitoshi kuondoa changamoto zinazowakumba wajasiriamali wanawake. Tunahitaji kuweka mazingira yanayowawezesha kwa kuwapa msaada wa kiufundi na kitaalamu kwa kuwakutunisha na wabobezi wa masuala ya biashara haswa katika ulimwengu wa kidigitali,” amesema.
Letitia Mswaki ambaye ni mjasiriamali amesema uwepo wa jukwaa hilo kutawasaidia wasichana waliokumbwa na ukatili wa kijinsia kupata msaada wa kisheria na kisaikolojia kwa urahisi bila ya malipo.