Wasiobadili umiliki vyombo vya moto wapewa siku 13

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka watu wote waliouziwa vyombo vya moto kufika katika mamlaka hiyo kabla ya Januari 20 mwaka huu ili kubadili umiliki huo.

TRA imesema kuanzia Januari 20 mwaka huu, itaanza kutumia mfumo wa kodi za ndani unaotambulika kwa jina la IRAS ambao hautaruhusu aliyeuziwa chombo cha moto kubadili umiliki, badala yake aliyeuza chombo hicho ndiye atakuwa na uwezo wa kubadili umiliki pekee.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Januari 7, 2025, Meneja Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Paul Walalaze amesema wamefikia hatua hiyo baada ya kubaini watu wanaonunua vyombo vya moto kutobadili umiliki.

“Mfumo wa sasa ukiwa na mkataba wa kisheria wa mauziano, hati ya kiapo, barua ya maombi ya kubadili jina na vitambulisho unabadilishiwa na hii ni kabla ya Januari 20,” amesema.

Walalaze amesema hatari iliyopo kwa mtu kutobadili umiliki wa chombo cha moto baada ya kununua ni kuingia matatizoni pindi chombo hicho kinapotumika kinyume cha sheria.

Ametolea mfano kesi ya mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, jina amelihifadhi akisema alikamatwa baada ya kubainika gari alilouza limehusika kusafirisha wahamaji haramu.

Pia, Walalaze amesema kutumia chombo cha moto bila kubadili umiliki ni kosa kisheria kwani kunaikosesha Serikali mapato.

“Makadirio ya kodi yameanza Januari hii na yanaisha Machi mwaka huu, watu wakifanya makadirio ya kodi unasema una gari moja, tukiangalia kwenye mfumo tunaona una gari, bajaji, lori tukikuuliza unasema ulishaviuza, kubadili sio kazi ngumu,”amesema.

Walalaze amesema utaratibu wa kubadili umiliki wa chombo cha moto TRA ni kupeleka kadi ya usajili wa chombo cha moto, mkataba wa mauziano na risiti ya EFD kutoka kwa mwanasheria aliyesaini mkataba huo au risiti aliyopewa wakati wa mauziano ya chombo husika.

Nyaraka nyingine ni kiapo cha umiliki, taarifa za muuzaji (picha na kitambulisho) taarifa za mnunuzi, barua ya maombi ya kubadili umiliki pamoja na kadi ya usajili na isainiwe na pande zote muuzaji na mnunuzi.

Dalali wa magari Ilala, Heri Saimon akizungumzia sababu ya baadhi ya wanaouza magari kuwa wagumu kubadili umiliki wanapouza ni historia ya gari lenyewe.

“Chombo kinaweza kuingizwa kwa magendo na kutengenezewa cheti feki, sasa mtu wa namna hiyo atauza gari kwa magumashi na atakuwa anamzungusha aliyemuuzia anapotaka kubadili atampa sababu ili tu asifanikiwe,” amesema.

Saimon amesema sababu nyingine ni nyaraka nyingi zinazohitajika ili kubadili umiliki wa gari nayo ni kikwazo kwani baadhi ya wamiliki hawana vitambulisho vya Taifa.

Related Posts