Na Nihifadhi Abdulla, Zanzibar
WATU wanaosadikika ni askari jamii wamedaiwa kumpiga Mwanamke na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko Bwejuu Wilaya ya kusini Mkoa wa kusini Unguja mhanga wa tukio hilo (jina limehifadhiwa) amesema tukio hilo limetokea mnamo Desemba 24, 2024 siku ya mkesha wa kumbukizi za sikukuu za kuzaliwa bwana Yesu Kristu Krismasi.
“Mimi nilikua natoka kwenye sherehe ya kuzaliwa ya rafiki yangu apo kwa LILA ndio akatokea huyo mwanamme akanipeleka Kwa wenzake na kuanza kunipiga Kwa kutumia waya wa umeme”
Amesema baada ya tukio hilo Kwa msaada wa wasamaria wema amefika kituo Cha polisi Paje na kupatiwa matibabu hospital ya Wilaya Kitogani.
Kwa upande wake rafiki wa aliekumbwa na tukio hilo Khadija Mohammed amesema kitendo hicho si cha kiungwana kwani kinanyima haki uhuru wa mtu hivyo ametoa wito Kwa Serikali kuwachukulia hatua waliofanya tukio hilo.
Nae Msaidizi wa sheria shehia ya Bwejuu, Asha Haji Awesu amesema uongozi wa Shehia inapaswa utoe elimu namna ya kupambana na kila wanalohisi halifai katika jamii na sio kuchukua sheria mikononi kuwaumiza wengine.
Ameongeza kuwa kitendo alichofanyiwa mwanamke huyo si cha kiungwana na ni udhalilishaji hivyo Serikali kusimamia vyema unyanyasaji huo kwani ukiachwa utapelekea kuzaa chuki na visasi visivyokuwa na tija.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kusini Unguja Daniel Shillah amesema anafuatilia tukio hilo na atatoa taarifa.