Waziri Mkuu wa Canada ajiuzulu kufuatia shinikizo za chama – DW – 07.01.2025

Hatua hiyo ya kujiuzulu imekuja miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa Canada. Justin Trudeau amesema anapanga kusalia kama waziri mkuu hadi kiongozi mpya wa chama atachaguliwa.

Trudeau alipoteza uungwaji mkono wa chama baada ya waziri wa fedha na mshirika wake wa karibu Chrystia Freeland kujiuzulu mwezi uliopita. Waziri Mkuu huyo wa Canada, mwenye umri wa miaka 53 alipoteza pia umaarufu miongoni mwa raia wake kufuatia kupanda kwa bei ya chakula, gharama ya makaazi na kuongezeka kwa wahamiaji. Lakini Trudeau amesema licha ya changamoto amefanya kila awezalo kwa ajili ya kuboresha maisha ya raia wa Canada.

“Tangu 2015, nimepigania nchi hii, ili kuimarisha na kukuza tabaka la kati, huku tukiungana kusaidiana kupambana na janga Corona, kuendeleza maridhiano, kutetea biashara huria katika bara hili, kusimama kidete na Ukraine na demokrasia yetu, na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na kuimarisha uchumi wetu kwa siku zijazo. Tuko katika wakati mgumu duniani.”, alisema Trudeau.

Chama tawala cha Kiliberali kinahitaji kumchagua kiongozi mpya kabla ya Bunge kuanza tena Machi 24. Lakini vyama vyote vitatu vya upinzani vinasema vitawasilisha kura ya kutokuwa na imani na serikali wakati wowote ule ili kuweko na uchaguzi wa mapema.

Vitisho vya Trump kwa Canada kujibiwa

Rais mteule wa Marekani Donald Trump alitishia kupandisha ushuru kwa asilimia 25 ya bidhaa za Canada
Rais mteule wa Marekani Donald Trump alitishia kupandisha ushuru kwa asilimia 25 ya bidhaa za CanadaPicha: Sean Kilpatrick/The Canadian Press/empics/picture alliance

Mivutano ya kisiasa imenakuja katika wakati mgumu kwa Canada. Donald  Trump anaendelea kuiita Canada kuwa jimbo la 51 la Marekani na ametishia kupandisha asilimia ishiri na tano ya ushuru wa bidhaa zote za Canada zinazoingia Marekani ikiwa serikali haitazuia kile Trump anaita “mtiririko wa wahamiaji na madawa ya kulevya nchini Marekani.”

Nchini kote, kujiuzulu kwa Justin Trudeau hakujawashangaza walio wengi. Mfano wa Rob Gwett, mkaazi wa mji wa Toronto ambaye amesema Trudeau alipaswa kujiuzulu zaidi ya mwaka mmoja uliopita, akiongeza kuwa tangazo la hivi sasa “limechelewa zaidi.”

Nani kumrithi Trudeau ?

Kwenye kura za maoni chama cha Kiliberali cha Justin Trudeau kimeonekana kupata pigo kubwa ikiwa uchaguzi utafanyika sasa, ikilinganishwa na chama cha upinzani cha Kihafidhina.

Vyombo vya habari vya Canada vimedokeza kuwa huenda waziri wa fedha aliyejiuzulu Chrystia Freeland akateuliwa kama kiongozi mpya wa chama tawala, au gavana wa zamani wa Benki ya Uingereza Mark Carney, raia wa Canada ambaye pia aliongoza Benki ya nchi hiyo.

Related Posts