Dar es Salaam. Mfanyabiashara na mkazi wa Kinondoni, Daud George (28) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuiba mita za maji na kuisababishia hasara ya Sh904,277. Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa).
Geoge amefikishwa Mahakamani hapo leo, Jumatano Januari 8, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka matatu.
Mshtakiwa huyo amesomewa mashtaka yake na wakili wa Serikali, Erick Kamala, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.
Wakili Kamala amedai katika shtaka la kwanza ambalo ni kuharibu miundombinu ya kutoa huduma muhimu, mshtakiwa anadaiwa Novemba 18, 2024 katika mtaa wa Mwananyamala Sindani, mshtakiwa aliharibu mita tatu zinazotumiwa kupima kiasi cha maji yanayotumika, mali ya Dawasa.
Shtaka la pili, siku na eneo hilo, George aliiba mita tatu za maji zenye thamani ya Sh904,277 mali ya Dawasa.
Shtaka la tatu, siku na eneo hilo mshtakiwa aliisabaishia hasara Dawasa ya Sh904,277 kwa kitendo chake cha kuiba mita hizo.
Upalelezi wa shauri hilo haujakamilika na mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote mahakamani hapo kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Hata hivyo, Hakimu Beda amesema dhamana ya mshtakiwa ipo wazi na mshtakiwa atapewa masharti ya dhamana na Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga ambaye ndio mhusika wa kesi hiyo.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Nyaki ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 21, 2025 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande.