Mwanza. Rajabu Reli (22) amehukumiwa miezi sita jela na Mahakama ya Wilaya ya Sengerema baada ya kukutwa na hatia ya kuvaa sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) bila ruhusa.
Hukumu hiyo ilitolewa jana Jumanne Januari 7, 2025 na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Evodius Kisoka katika shauri la jinai namba 445 la mwaka 2025.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Nyamhanga Tissoro mshtakiwa alitenda kosa hilo Desemba 5, 2024 katika Kijiji cha Kasisa, wilayani Sengerema kinyume na kifungu cha 178(1) cha sheria ya kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani Januari 7, 2025 na kusomewa shtaka la kuvaa sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania bila ruhusa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya kusikiliza pande zote za ushahidi, Hakimu Evodius Kisoka alijiridhisha ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri haukuacha shaka lolote.
Mahakama ilipompa nafasi ya kujitetea, mshtakiwa aliiomba imuachie huru kwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na alivaa ili akubaliwe na mchumba wake.
“Mheshimiwa Hakimu naomba nisamehewe kwa kuwa ni kosa la kwanza na nilivaa na kwenda kumuonesha mchumba wangu kuwa mimi ni askari ili asinikatae,” aliomba Rajabu.
Hata hivyo, ombi lake lilitupiliwa mbali na Hakimu Kisoka na kumhukumu miezi sita jela ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama yake.